MWANDISHI Mkongwe na Mchambuzi wa siasa Jenerali Ulimwengu amewataka wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini kushirikiana na waandishi wao katika mapambano dhidi ya Uhuru wa Habari.
Ulimwengu amesema wamiliki wa vyombo vya habari wanatakiwa kujua kwamba licha ya kuwa wamiliki wa vyombo hivyo lakini lengo kuu ni kuhudumia jamii .
Akizungumza jijini Dodoma katika mjadala wa wamiliki wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA TAN),Ulimwengu amewataka wamiliki hao kutokuwa sehemu ya ukandamizaji wa Uhuru wa habari kwa maslahi yao binafsi.
“Kuna watu wanaanzisha vyombo vya habari lakini lengo ni kulinda itikadi zao za kisiasa maslahi ya biashara zao au marafiki zao wanasahau kwamba vyombo wanavyoanzisha ni mali ya wananchi,kwa sababu vyombo vyote vinaanzishwa ili kuhudumia wananchi.” Alifafanua Ulimwengu.
Jenerali amesema kwa kipindi cha miaka kadhaa nyuma tasnia ya habari imekuwa mfu kutokana na sababu mbalimbali lakini amesema wamiliki wa vyombo vya habari hawawezi kukwepa kudorora huko kwa tasnia muhimu katika jamii.
Ulimwengu amewataka wamiliki ambao kama wanaona hawapo tayari kufanya na kuhudumia jamii ni bora wahamishie mitaji yao katika shuguli nyingine ili kuacha nafasi hiyo kwa watu wenye nia ya dhati ya kusaidia kupaza sauti za wananchi ili kutatua changamoto zinazowakabili.
“Kama una chombo cha habari na hakiwajibiki kwa wananchi ni bora ukafanye kazi nyingine,kazi ya habari inabidi ujikane hadi nafsi yako na kuwa ‘commited’ kwenye kufanya kazi hiyo.” Amesema.
Hata hivyo Ulimwengu amewashauri wamiliki hao kuweka utaratibu mzuri utakaowawezesha waandishi wao kujiendeleza kielimu ili kuongeza maarifa yatakayowasaidia kuchakata kwa weledi maudhui wanayoyapeleka kwa hadhira yao.
Kwa upande wake Mhariri Mwandamizi mstaafu Jesse Kwayu amewataka wamiliki kushirikiana na watendaji wao (waandishi) ili kuweza kurudisha heshima ya vyombo vya habari nchini kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
“Vyombo vya Habari kwa sasa haviogopwi kama zamani,Wamiliki ni lazima kushiriki katika harakati za kurudisha vyombo vya habari kurudisha ‘lost glory’ (heshima iliyopotea) katika tasnia ya habari” amesema Kwayu.
Kwa upande wao wamiliki wa vyombo vya habari wameibua changamoto mbalimbali ambazo zikirekebishwa zinaweza kurudisha heshima katika tasnia ya habari.
Mmiliki wa Standard FM (Singida) Daudi James amesema tabia ya waandishi wa habari kuendekeza ‘bahasha ya kaki’ (posho) imekuwa tatizo kubwa katika kutengeneza maudhui yasiyo na faida kwa jamii zaidi ya kumtangaza yule aliyewalipa posho.
“Bahasha(posho) zinatuulia vyombo vya habari,waandishi wengi hawaandiki habari za uchunguzi wanakimbilia kwenye habari zenye posho tu.” Amefafanua mmiliki huyo.
Kwa upande Abdul Diallo akimuwakilisha mmiliki wa kampuni ya Sahara Media Group amesema baadhi ya Wahariri na Waandishi wanashiriki kuminya uhuru wa habari kutokana na kuendekeza itikadi zao za kisiasa.
Dialo amesema katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita wapo baadhi ya Wahariri na waandishi waandamizi waligombea nafasi mbalimbali katika vyama vya siasa,amesema tukio hilo lilidhhirisha kwa namna gani waandishi wenyewe wana pande ambazo wanazitumikia.
“Kuna wamiliki ni wanasiasa lakini hawaingilii vyombo wanavyovimiliki lakini kuna baadhi ya matukio ya uminywaji wa uhuru wa kujieleza tatizo ni itikadi za wahariri wa habari wamiliki hawatakiwi kulaumiwa”alifafanua Dialo.
Mjadala huo umefanyika wiki hii ukiwa na lengo la kuwajengea uelewa wamiliki wa vyombo vya habari kuhusu kazi ya vyombo vya habari kwenye kuchochea uwazi, haki na demokrasia.
Lengo jingine la mjadala huo kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoathiri uhuru wa kiuhariri unaosababisha kutokuwepo kwa uhuru wa kiuhariri kwenye vyombo vya habari unapelekea vyombo vya habari kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kusaidia jamii.