Kamishna wa Ardhi , Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Nathaniel Nhonge
Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, Dodoma
KAMISHNA wa Ardhi , Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Nathaniel Nhonge amewataka watanzania kulipa kodi ya pango la ardhi kabla ya Januari Mosi mwakani ili kuepuka riba ya asilimia moja ambayo watatozwa kila mwezi kama faini endapo watachelewa kulipa kodi hiyo.
Hayo yameelezwa leo Alhamis Desemba 30,2021 Jijini Dodoma na Kamishna huyo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kodi ya pango hilo la Ardhi ambapo amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni maendeleo .
Kamishna Nhonge amesema watanzania wengi wameitikia wito wa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa mwaka huu hivyo amewataka kuendelea kulipa kwani ifikapo Januari mosi mwakani watatakiwa kulipa faini ya riba ya asilimia moja kwa mwezi.
“Kwa maana ikifika tarehe moja mwezi wa kwanza kwa maana ile kodi yako inaanza na riba sisi msisitizo wetu ni kilipa kipindi hichi cha miezi sita ambayo haina riba sasa kila mwezi sasa inaanza kuongezeka tunaona ni muhimu kuwaambia wananchi muda upo baada ya tarehe 31 tutaanza kutoza na riba,”amesema.
Aidha Nhonge amesema Wizara hiyo imeweka utaratibu mzuri ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za ulipaji kodi ambapo wameanzisha kituo cha mawasiliano kwa wateja na wanaweza kuwahudumia wananchi popote walipo ili kuwawezesha kulipa kodi.
Vilevile amesema mikakati ya Wizara hiyo ni kuhakikisha ina pima ardhi kwa kasi ili kila Mtanzania aweze kumiliki ardhi ambapo tayari Wizara hiyo ilishapokea fedha kiasi cha Shilingi bilioni 50 kutoka Serikalini kwa ajili ya kazi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha kodi Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya Makazi Denis Masami amesema kuwa katika kipindi cha kuelekea mwisho wa mwezi mwitikio wa ulipaji kodi ya pango la ardhi umeongezeka na wengi wamejitokeza kulipa.
Amesema hadi sasa wameshakusanya kiasi cha Shilingi bilioni 60 na malengo ni kukusanya bilioni 221.
“Sasa hivi ukusanyaji umeongezeka kwa wiki tunakusanya bilioni 2 mpaka 4 kwa Jiji la Dodoma kwa mwaka huu kulikuwa na wamiliki 250 waliokuwa wanalipa lakini sasa hivi wamiliki ni 890 kwa wiki hata kiwango tulichokuwa tunakusanya kilikuwa milioni 60 mpaka 70 sasa hivi mpaka milioni 200",amesema.