KIJANA, Hamad Ali Hamad (25) mkazi wa Chake Chake, Pemba ameanza kutumikia kifungo cha miaka 14 gerezani baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya kubaka na kutorosha msichana mwenye umri wa miaka 14.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu wa Mahakama ya Chake Chake, Abdallah Yahya Shamuhuna.
Awali akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya DPP, Juma Mussa alidai mshtakiwa alimchukuwa binti huyo aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake na kumpeleka nyumbani kwake, jambo ambalo ni kosa chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Alidai kitendo cha kumtorosha binti huyo na kumuweka nyumbani kwake, kwa kiasi kikubwa kimesababisha usumbufu kwa wazazi wake pamoja na kumkosesha kwenda shule kwa muda.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Shamuhuna alisema ameridhishwa na upande wa utetezi ukiongozwa na mashahidi saba na kumtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kosa la kutorosha na kumbaka binti huyo ambaye yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake.
“Kubaka ni kosa kwa mujibu wa sheria chini ya mwenendo wa makosa ya jinai, ambapo mtuhumiwa atatumikia chuo cha mafunzo (gerezani) miaka 14 na kumlipa fidia muhusika Sh milioni 2,” alisema hakimu huyo.
Serikali ya Zanzibar imeanzisha mahakama maalumu ya udhalilishaji wa kijinsia na kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu imewatia hatiani washtakiwa 20 na kuwahukumu kifungo cha miaka 14 hadi 30, huku kesi zikisikilizwa kwa haraka.
Social Plugin