Na
Adeline Berchimance, KIGOMA
SERIKALI itaendelea
kuweka mazingira mazuri na uwekezaji katika Sekta ya Mawasiliano ili iweze
kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuchochea shughuli za maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa
akizindua mnara wa Mawasiliano katika
Kijiji cha Kasumo Kata ya Kajana Wilaya ya Buhigwa mkoani Kigoma.
Alisema mnara huo ni sehemu ya mkakati wa
Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana
nchi nzima na kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wanaoishi pembezoni na
hasa vijijini waweze kumudu matumizi ya huduma hiyo.
Alisema ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Kasumo ni mwendelezo wa
jitihada za Serikali kuufungua Mkoa wa Kigoma na kuwezesha wananchi kutumia
huduma za intaneti, ambazo pia zitaboresha huduma za kijamii na kufungua fursa
za kiuchumi.
Mhe. Dkt. Mpango amewaeleza wananchi fursa zitakazopatika kutokana
na matumizi ya intaneti na mawasiliano ya simu kwa ujumla ni pamoja na
kuwaunganisha wananchi wa Kata ya Kajana, Kata ya Muyamba na Vijiji jirani, pia
kuunganishwa na masoko ya mazao yanayozalishwa katika Wilaya hiyo na biashara
mbalimba zinazofanyika katika Wilaya hiyo.
“Mtandao wa simu unatuwezesha kuongeza na kupanua mtandao wa Wateja
na hivyo kurahisisha shuguli mbalimbali za kiuchumi,” alisema Dkt. Mpango.
Aidha amebainisha kuwa kupitia mnara huo wananchi wataweza kuwasiliana moja kwa moja na vyombo vinavyotoa huduma muhimu za kijamii, pamoja na kupata ushauri kutoka kwa wataalam wa kilimo, ufugaji na kuboresha shughuli zao, huku Wanafunzi wa Shule za Msingi hadi vyuo kunufaika pia kwa matumizi ya intaneti kujisomea na kujipatia maarifa mapya.
Kwa kuzingatia faida na fursa zinazopatikana katika huduma ya
mawasiliano, Dkt. Mpango amewataka wananchi wa Kijiji cha Kasumo na Wilaya
nzima ya Buhigwe kulinda na kutunza miundombinu hiyo kwani imegharimu fedha
nyingi za Serikali.
Amesema uharibifu wa miundombinu hiyo italeta hasara na madhara
makubwa kwa wananchi wa Buhigwe na Kasulu kiuchumi na kijamii
“Ukiharibiwa huu mtambo maana yake tutakosa huduma ya mawasiliano
pamoja na faida zote za huduma hii zitapotea na hivyo kurudisha nyuma juhudi za
serikali za kuwaletea maendeleo,” alisema Dkt. Mpango.
Aidha amewataka Wanachi hao kutumia vyema huduma hii na kujiepusha
na matumizi mabaya ya mitandao ikiwemo kutazama na kusambaza picha ambazo
hazina maadili kulingana na tanaduni za kitanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amelipongeza Shirika la Mawasiliano -TTCL kwa kushirikiana
na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote –UCSAF kwa kufikisha huduma ya mawasiliano ya
uhakika kwa wakazi wanaoishi katika kijiji cha cha kasumo pamoja na vijiji
jirani.
Amesema mnara huo utatoa huduma ya Intaneti kwa kazi ya 4G ambayo
imekuwa ni hitaji msingi kwa maisha ya mwanadamu katika dunia ya sasa na kwamba
mnara huo unaenda kufanikisha agenda ya serikali ya kufikisha huduma ya
intaneti hadi ngazi ya vijiji.
Alisema pamoja na ujenzi wa mnara huo Wizara yake ipo katika
mkakati wa kufikisha Mkongo wa Taifa mpaka Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe
katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.
Alisema Mkongo huo utarahisisha Zaidi huduma ya intaneti
zilizofikishwa na mnara huo kwa bei nafuu Zaidi kwa wananchi wa Wilaya ya
Buhigwe na Kigoma nzima ili kujenga uchumi wa kidigitali.
Alisema Mradi huo uliozinduliwa ni sehemu ya miradi ya mawasiliano
vijijini inayotekelezwa kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ambapo mpaka sasa
TTCL kwakushirikiana na UCSAF imeishajenga minara katika Kata 171 zinazojumuhisha vijiji 381.
Alisema TTCL imeendelea kubeba dhamana ya usimamizi na uendeshaji
wa miundo mbinu ya kimkakati ya mawasiliano, kiufundi na kibiashara ikiwemo
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo Mahili cha Kuhifadhi Data yaani.
Alisema miundo mbinu hii imekuwa na matokeo chanya kwenye
maendeleo ya Taifa ambapo mpaka sasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umefika
katika nchi zilizoko katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Akisoma taarifa ya Mradi wa Mnara huo Mkurugenzi Mkuu Shirika la
Mawasiliano Bw. Waziri Kindamba alisema mradi huo umekamilika katika kipindi
cha miezi miwili huku ukigharimu shilingi 326,874,773.75.
Bw. Kindamba alisema TTCL imetoa shilingi 208,624,772.75 huku Serikali
kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ikitoa kiasi cha shilingi
118,250,000.00.
Alisema mnara huo una uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano ya Intaneti, Ujumbe
Mfupi na Dakika (Voice) kwa teknolojia ya kisasa ya 4G, kubwa zaidi wananchi
watapata fursa ya kutumia huduma za Intaneti yenye kasi zaidi.
Alisema kuwa huduma hii ya mawasiliano italeta mageuzi makubwa katika Kata ya Kajana kutokana na uwepo wa fursa mbalimbali kiuchumi na kijamii ikiwemo kuondoachangamoto ya Mawasiliano na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi kuweza kujipatia kipato kupitia uwakala wa huduma mbalimba za TTCL na Kampuni tanzu ya T-PESA.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Bi Justina Mashiba alisema jukumu kubwa la Taasisi yake nikuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini na mipakani mwa nchi wanapata huduma za mawasiliano.
Alisema UCSAF imejipanga vizuri kuhakikisha
kila Mtanzania anayeishi Kijijini au maeneo ya pembezoni anapata huduma za
mawasiliano.
“maeneo ya mipakani ni sehamu ambazo zinahitajika kulindwa kwa ajili ya usalama wa nchi yetu hivyo ni jukumu la UCSAF kuhakikisha maeneo hayo yanalindwa na Watanzania wanaishi na kufanya shughuli zao katika maeneo hayo wanapata huduma za mawasiliano,” Alisema.