Jeshi la Polisi mkoani Njombe linamshikilia mkazi mmoja wilayani Ludewa majina yanahifadhiwa kwa sababu ya uchunguzi, akituhumiwa kuhusika na mauaji ya mtu mwenye umri wa miaka 34 mkazi wa Kijiji cha Njelela wilayani humo na kulipwa pesa kiasi cha Tsh 40,000 kati ya Tsh 100,000 alizoahidiwa kwa kutekeleza mauaji.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Hamis Issa amesema polisi walikwenda kuangalia tukio na kukuta mtu amefariki na marehemu alikuwa na pikipiki yake baada ya kuuawa,muuaji akachukua Pikipiki ya marehemu na kutembea nayo mjini.
“Muuaji alichukua pikipiki ya marehemu na kutembea tembea nayo mjini na kukamatwa nayo alipoulizwa yeye alidai amepewa kazi ya kuua huyu na kupewa Tsh 40,000 bado Tsh 60,000 na kweli tuliweza kumtafuta mtu aliyetoa hela hiyo naye tumemkamata hayo ni mafanikio,” amesema Kamanda Issa.
Kamanda Issa ametoa wito kwa jamii kuacha kupokea fedha ili kufanya uhalifu wa kuua au kumsababishia mtu apate matatizo ya aina yoyote ile sambamba na kuacha kukodiwa kwa jambo lolote baya.
“Eti tunamuoji kwanini mmemuua anasema walikuwa wanagombea mashamba na kama mnagombea mashamba sheria zipo.Tunashauri wanaNjombe fuateni sheria acheni kujichukulia sheria mikononi kitu ambacho ni tatizo kubwa ambalo linaweza likaleta madhara katika jamii nzima,” amesema Kamanda Issa.