MGEJA AIPONGEZA SEKRETARIETI YA CCM KWA KAZI NZURI



Khamis Mgeja

Na Baltazar Mashaka,Kahama

SEKRETARIETI ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),chini ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chama, Daniel Chongolo, imepongezwa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Chama,ufuatiliaji na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025.

Pongezi hizo zilitolewa jana na mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM,Khamis Mgeja, wakati akizungumza na wazee wa Chama waliomtembelea kijijini kwake Nyanembe, wilayani Kahama, kubadilishana mawazo na kujionea shughuli za kilimo anazofanya.

Wazee hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Charles Gishuli, pamoja na mambo mengine walizungumzia mustakabali wa nchi hasa hali ya kiuchumi,kisiasa na kijamii.

Katika mazungumzo hayo wazee hao walikiri kwa sasa nchi inakwenda vizuri katika masuala ya maendeleo, kiuchumi na amani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu hali kisiasa ndani ya CCM Mgeja ambaye ni kada mkongwe katika siasa nchini alitumia fursa hiyo kuwaeleza wazee hao (makada)kwa namna utendaji wa Sekretarieti ulivyo na inavyoupiga mwingi chini ya Chongolo.

“Sote tunaona sekretarieti inavyozunguka kwenye mikoa mbalimbali ,wilaya, kata,matawi na mashina ya Chama,wanafanya kazi kubwa na nzuri inayopaswa kuungwa mkono na wana CCM pamoja na watu wengine wenye mapenzi mema na kinachofurahisha wametembelea wanachama kwenye mashina na miradi ya maendeleo kuona ilani ya uchaguzi inavyotekelezwa,”alisema Mgeja.

Alisema Chama kimekuwa kikitoa maelekezo kwa serikali ili kushughulikia na kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi na kuhakikisha zinatafutiwa ufumbuzi kuondolewa ikizingatiwa CCM ndiyo yenye dhamana ya kuongoza nchi.

Mgeja ambaye amepumzika siasa kwa muda awaambia wazee hao kuwa ile CCM waliyokuwa wakiifahamu siku za nyuma sasa inaonekana kwenye utendaji wa sekretarieti chini ya utendaji makini wa Katibu Mkuu (Chongolo) anavyofanya kazi ndani na nje ya Chama na kwenye umma ‘kuna kazi ndani ya Chama na nje ya Chama na ndani ya umma’.

“Pongezi za pekee ziende kwa Halmashauri Kuu chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wake makini wa sekretarieti ya watendaji hodari wenye weledi wanaotokana na CCM, sote tunafahamu wote wamelelewa na kukulia keenye Chama wala hawakuibuka kama uyoga ndani ya CCM,”alisema.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliendekea kuipongeza sekretarieti hiyo akisema si ya kutoa maagizo na kubaki kukaa tu ofisini na kugeuka kuwa mangimeza, ni sekretarieti inayofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inakijenga Chama na kukijengea imani kwa wananchi kuwa CCM ndiyo tegemeo na kimbilio la wanyonge, kwa hakika Chama kimepata watendaji wazuri na si watendaji wamekipata Chama.

Hata hivyo, Mgeja alitoa masikitiko yake yaliyojaa mshangao kuwa sikuza karibuni kulizuka maneno manebo yasiyofaa ya CCM mpya, yalitaka kuwagawa wana CCM na kuonyesha wapo wanaoonekana bora na wasio bora.

“Maneno hayo ya CCM mpya yalijaa ubaguzi, katika siasa wote ni muhimu na wanategemeana, hakuna bora zaidi ya mwingine na aote tuna fahamu CCM ni ile ile ya zamani iliyoyokana na vyama vya TANU na ASP,”alieleza Mgeja.

Kwa upande wake, Gishuli alisistiza mshikamano,upendo na umoja ndani ya Chama kwa sababu ziara za sekretarieti zinachangia kuhuisha mshikamano na zinawafanya wana CCM wawe wa moja badala ya kufarakana na kugawanyika.

Pia aliwaasa Watanzania na wana CCM kujenga mshikamano wa kitaifa, wamuunge mkono Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ilani ya CCM 2020-2025 kwa kiwango cha hali ya juu huku wakuendelea kulinda misingi ya amani na utulivu.

“Bila amani katika nchi yetu, maendeleo ni sawa na debe shinda haliachi kutika, tuendelee kushikamana,kushirikiana na kudumisha amani ya nchi yetu,”alisema Gishuli.

Pia kwa niaba ya wazee wenzake, alimpongeza Mgeja kwa uamuzi wa busara alioufanya baada ya kumpunzika siasa kwa muda na kujielekeza kwenye kilimo, anatekeleza ilani kwa vitendo na kufuata nyayo za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwa vitendo kwani baada ya kung’atuka naye alibaki kujishughulisha na kilimo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post