MARY MASANJA AWATAKA WAKUU WA WILAYA KUHIFADHI MAENEO YA URITHI WA UTAMADUNI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Mary Masanja (Mb) akikabidhiwa zawadi ijulikanayo kama nyengo katika ufunguzi wa Siku ya Utamaduni wa Mtanzania katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.Baadhi ya washiriki wa Siku ya Utamaduni wa Mtanzania wakifuatilia matukiao katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Mary Masanja (Mb) akizindua Siku ya Utamaduni wa Mtanzania Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

******************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kutathmini na kutafuta maeneo ya utamaduni yenye historia nzuri na kuanzisha makumbusho zitakazoweka kumbukumbu za utamaduni wa eneo husika na kuelezea historia ya jamii hiyo.

Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Siku ya Utamaduni wa Mtanzania iliyowakilishwa na Jamii ya Wanamakete katika Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

“Niwaombe sana viongozi wa Serikali hasa wakuu wa wilaya na Halmashauri kwenye maeneo yenye historia nzuri basi tuzitafute ,tuzitunze na kuanzisha makumbusho” Mhe. Masanja amesisitiza.

Ameongeza kuwa endapo Watanzania watadumisha, kuendeleza na kuthamini tamaduni zao utalii utaendelea kukua zaidi.

“Mataifa mengi yamepata mapato kutokana na utalii wa utamaduni sisi pia tukiendeleza maeneo haya na kuyathamini mapato yataongezeka” Mhe. Masanja amesema.

Aidha, Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa kupitia matamasha ya utamaduni elimu hutolewa kwa vijanaili wafahamu ni wapi jamii yao imetoka, inaenda na na pia kuzidumisha mila,desturi na tamaduni husaidia kuwaunganisha Watanzania.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amewaasa Watanzania kutumia matamasha ya utamaduni kufanya majadiliano ya kimaendeleo ili kuunga mkono jitihada za Serikali zinazohimiza wananchi kujikwamua katika hali ya umaskini, ujinga na maradhi.

Mhe. Masanja pia ameipongeza Bodi ya Makumbusho ya Taifa kwa kubuni mpango huo wa kufanya matamasha ya kiutamaduni lakini amewataka kuhamasisha jamii nyingi zaidi ziweze kushiriki katika matamasha hayo.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Christowaja Ntandu ameahidi kuendelea kushirikiana na Jamii ya Wanamakete ili kuhifadhi utamaduni wa jamii hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post