Baadhi ya washiriki katika Kongamano la Tathmini ya hali ya Haki za binadamu ndani ya miaka 60 ambalo limefanyika leo jijini Dar es salaam.
......................................
NA MUSSA KHALID,DAR ES
SALAAM
Katika kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa
Tanzania Bara,Serikali imesema itaendelea kukuza na kuendeleza haki za binadamu
katika makundi mbalimbali pamoja kuboresha maendeleo nchini ili watanzania
waweze kuzipata haki zao kwa wakati.
Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam
na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Amon Mpanju wakati akifungua Kongamano la Tathmini ya hali
ya Haki za binadamu ndani ya miaka 60 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ambalo limeandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) pamoja
na Wizara ya Katiba na Sheria.
Naibu Katibu Mpanju
amesema ni vyema waTanzania wakashirikiana na serikali katika kusimamia haki
zao katika kuleta maendeleo nchini kwani jambo kuzilinda haki za binadamu sio la
serikali pekee bali ni la watu wote.
‘Ukiangalia toka mwaka
1961 tunapata uhuru viongozi wetu hususani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
aliweka misingi iliyozingatia haki za binadamu utaona kauli alizokuja nazo za
kupambana na ujinga,umaskini na maradhi ililenga kuhakikisha wananchi
wanawezeshwa kiuchumi kwa kupata elimu na huduma za afya’amesema Mpanju
Awali akizungumza Mratibu
Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC ) Onesmo
Olengurumwa amesema wameamua kuwa sehemu ya miaka 60 ya uhuru hivyo wamefanya
tathmini ili kuangalia haki kwani ndio kiungo muhimu katika uhuru wa nchi.
‘Katiba yetu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendeshwa kwa misingi ya haki na utawala bora
hivyo yote yapo katika katiba yetu na tumekuwa tukiyafanyia kazi’amesema
Olengurumwa
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Jaji Mstaafu Mathew
Mwaimu amesema kuelekea kuadhimisha Dec 10 siku ya haki za binadamu ni vyema
ikaendelea kufanywa tahmini ya kuzisimamia haki za binadamu ili kutoka katika
changamoto na kusaidia wananchi kupata haki zao.
Amesema katika miaka
60 ya uhuru yapo mambo mbalimbali ambayo yamefanywa na Serikali,Asasi za Kiraia
pamoja na wadau wengine wa haki za binadamu na maendeleo hivyo ameeleza
kufanywa tathimin kila baada ya miaka itasaidia kuweka mazingira mazuri kwa
watanzania.
Naye Mwenyekiti wa Chama
cha Siasa nchini cha NCCR Mageuzi James Mbatia amesema suala la haki za
binadamu linapaswa kuzungumzwa mara kwa mara ili haki mbalimbali zikiwemo haki
ya kusikiliza,Utu wa mwanadamu,haki za kuweza kuishi zikaonyesha mazingatio.
Mdahalo huo umewashirikisha wadau mbalimbali maarufu nchini akiwemo Aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) Dkt Hellen Kijobisimba,Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar na mabalozi kutoka maeneo mbalimbali.