TAASISI ya vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara (Media Institute of Southern Africa - MISA Tanzania) imekutanisha waandishi wa habari na wadau wa habari mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu sheria mbalimbali za habari za vyombo vya habari nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jana katika Hoteli ya Gentle Hill mjini Iringa Kaimu mkurugenzi wa MISA Tanzania Andrew Marawiti alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo MISA Tanzania imeendelea kutoa kwa wana habari wa mikoa mbali mbali nchini lengo ni kuwajengea uwezo wa kutambua na kuchambua sheria hizo pamoja na kutoa maoni yao.
Alisema kuna changamoto ya mwitikio kutoka kwa waandishi kujitokeza ipasavyo katika kupaza sauti kujitetea wenyewe juu ya sheria hizo ili pale inapowezekana ziweze kufanyiwa marekebisho ili zisiwe mwiba kwa wahabari na vyombo vya habari .
“Maslahi ya mwana habari yatatetewa na mwandishi mwenyewe hivyo waandishi ni jukumu letu kujitambua na kupaza sauti juu ya matatizo na changamoto zinazo tukumba katika utendaji kazi wetu nia ni kuifanya tasnia ya habari ikue na iheshimike”,alisema.
Alisema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi hao ili kutambua maudhui ya sheria hizo.
“Tunachofanya kupitia mafunzo haya ni kuwaonesha na kuwasaidia Waandishi wa Habari wapate uelewa wa sheria ambazo zinasimamia tasnia yao”,aliongeza
Alisema kuwa kupitia mafunzo hayo waandishi watakuwa na uwezo wa kushiriki mijadala mbalimbali ikiwemo ile ya mabadiliko ya baadhi yaa vifungu katika sheria hizo ambazo zinaonekana kuminya uhuru wa kujieleza.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo mwanahabari mkongwe Jesse Kwayu alisema kwenye sheria hizo kuna mambo mengi mazuri lakini mazuri hayo yanafunikwa na vifungu vichache vinavyominya uhuru wa habari na kujieleza.
Kwayu aliwataka waandishi wa habari kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili wawe na uelewa juu ya vifungu mbalimbali katika sheria hizo.
“Sheria tulizonazo ukizisoma kwa wepesi utaziona ni nyepesi lakini ni sheria nzito sana,na Mwandishi ili akamilike lazima azifahamu sheria hizi ..sheria hizi zipo nyingi ila kutokana na utendaji kazi tutajikita katika sheria tatu ambazo sheria ya vyombo vya kielektroniki “EPOCA”, sheria ya takwimu “STATISTICS ACT” na sheria ya vyombo vya habari “MEDIA SERVICE ACT 2016”,alisema Jesse Kwayu.
Alisema sheria hizi zimekuwa zikilaumiwa kuwa zinakinzana na uhuru wa habari kwa mwandishi wa habari hivyo lengo kubwa ni kutoa uelewa waandishi wa zijue sheria hizo na ipaze sauti ili ziweze kufanyiwa marekebishpo kwa ustawi wa tasnia ya habari
Kwa upande wake mdau wa habari kutoka Asasi ya kiraia ya ICISO mkoani Iringa Raphael Mtitu aliwataka waandishi wa Habari kushirikisha taasisi za kiraia katika mapambano ya kudai haki kujieleza kwa vile ni matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema haki hiyo inamgusa kila mwananchi hivyo ni vyema taasisi zote zikaungana kupigania haki hiyo.
“Msione hili jambo ni kwenu peke yenu,kama hivi MISA TAN walivyotushirikisha basi iwe fursa kwa taasisi nyingine za habari kuona umuhimu wa kushirikisha taasisi za kiraia ili kuunganisha nguvu na kuwa sauti ya pamoja” ,alisema Mtitu.
"Tuungane pamoja katika harakati za kudai uhuru wa habari,linapomtokea mwenzako leo kesho linaweza kuwa kwako.Mmoja wetu akipatwa na tatizo tusiiache MISA Tanzania pekee",aliongeza.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo,wamewataka waandishi wa habari wote kuungana pamoja katika kutetea maslahi ya tasnia.
Denis Nyali ambaye ni mmoja kati ya walioshiriki warsha hiyo alisema kuna mambo mengi yanayosonga utendaji wa wanahabari nchini lakini kwa mara kadhaa waandishi hawatoi ushirikino katika kutatua changamoto za wenzao.
Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari Iringa (IPC) Frank Leonard akichangia maoni yake alisema miongoni mwa sheria zinazokiuka uhuru wa waandishi ni sheria inayowataka waandishi kuanza kutambulika kuanzia ngazi ya Stashahada ya Habari na kuendelea
“Kuna waandishi wa habari wana Shahada moja wengine mbili lakini ukiwaambia waandike story (habari) hata paragraph moja hawawezi huu ni mtihani lakini wapo ambao wana cheti tu na wana uwezo wa kuandika stori nzuri kabisa ambayo ni zaidi hata ya huyu mwenye elimu kubwa amesema” alisema Leonard.
Huku washiriki wa mjadala huo wakitamani sheria ipitishwe kwa mtu kuwa mbunge lazima awe na kiwango cha elimu kuanzia Diploma kama wanahabari ili awe na utashi mkubwa wa kuchambua na kutunga sheria mbalimbali za nchi .
"Wabunge wanapitisha sheria ya kikomo cha elimu kwa wanahabari kuwa ni Diploma wakati ili mtu uwe mbunge kigezo kikubwa ni kujua kusoma na kuandika na kuwa ingependeza na wao wabunge kigezo cha elimu kitiliwe mkazo",walisema
Naye mwanahabari Ibrahim Kitang’ala alisema kuwa sheria hizi nyingi zinapitishwa na wabunge ambao kigezo chao cha kuwa mbunge ni walau awe na elimu ya darasa la saba tu.
“Unakuta mbunge ana elimu ya darasa la saba halafu anapitisha sheria mwaandishi wa habari niwe na Stashahada huyu wa darasa la saba anajuaje stashahada”, alisema Kitang’ala.
"Kuwa wabunge wanapitisha sheria ya kikomo cha elimu kwa wanahabari kuwa ni Diploma wakati ili mtu uwe mbunge kigezo kikubwa ni kujua kusoma na kuandika na kuwa ingependeza na wao wabunge kigezo cha elimu kitiliwe mkazo",aliongeza
Social Plugin