Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limemuokoa mtoto mchanga wa kiume anayekadiliwa kuwa na umri wa siku mbili hadi tatu aliyekuwa ametupwa katika shimo la choo linalokadiliwa kuwa na urefu wa mita zaidi ya 20 la Shule ya Msingi Rukajange iliyopo kata ya Bugene Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Mtoto huyo alibainika Desemba Mosi, 2021 wakati mwalimu wa shule hiyo, George Ishoko alipokuwa akipita kilipo choo kusikia sauti ya mtoto ikitokea ndani ya shimo na kutoa taarifa ofisi za Zimamoto waliofika eneo hilo na kumtoa.
Kaimu mkuu wa jeshi hilo Wilaya ya Karagwe, Karata Ramadhan Karata amesema mtoto huyo alikuwa amefungwa kwenye mfuko na kitambaa cheusi.
Amesema mtoto huyo amelazwa hospitali teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga kwa ajili ya matibabu na uangalizi wa madaktari.
Mganga mkuu katika hospitali hiyo, Dkt. Furaha Kahindo amesema hali ya kichanga hicho inaendelea vizuri na leo anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali na atakabidhiwa kwa mama ambaye ameomba kumnyonyesha baada ya kukubaliwa na mamlaka aishi naye.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo mwalimu katika shule ya msingi Rukajange, George Ishoko amesema kuwa, wakati akiwa anapita karibu na choo hiyo alisikia sauti ya kichanga hicho.