Mwalimu wa Shule ya Msingi Magemo iliyopo Webuye, Kaunti ya Bungoma nchini Kenya, Wycliffe Akeve amejichoma kwa moto katika jaribio la kujiua, baada ya kufukuzwa kazi kwa madai ya kumpa ujauzito mwanafunzi wake.
Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Mji wa Webuye, Peter Yego amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba mwalimu huyo, alijaribu pia kuwachoma kwa moto walimu wenzake, baada ya kujifungia kwenye chumba cha ofisi ya walimu na kufanya tukio hilo.
Kwa mujibu wa mmoja kati ya walinzi wa shule hiyo, Akeve alifika shuleni hapo Desemba 17, 2021 majira ya saa moja za asubuhi na kwa kuwa tayari alikuwa amekabidhiwa barua ya kufukuzwa kazi, aliingia kwa kupitia mlango wa nyuma.
Baada ya kuingia shuleni hapo, mwalimu huyo alionekana akizungumza na walimu wenzake na muda mfupi baadaye, aliingia katika ofisi ya walimu na kufunga mlango kwa ndani huku kukiwa na walimu wengine na kujaribu kujilipua kwa moto kwa kile kinachodaiwa kwamba ni kutorodhishwa na uamuzi uliofikiwa na mwajiri wake wa kumfukuza kazi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi nchini Kenya, mwalimu huyo aliokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Bungoma anakoendelea na matibabu baada ya kupata majeraha ya moto na atakapopona, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kujaribu kujiua, kujaribu kuwaua walimu wenzake na uharibifu wa mali.
Social Plugin