







******************
MEYA Mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda amekabidhi jezi kwa timu nane zilizofuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Mwenda Cup inayoendelea kufanyika Mikocheni katika Wilaya ya Kinondoni.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya inayojihusisha na masuala mbalimbali ya kijamii ya Mwenda Foundation yamehusisha jumla ya timu 16 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yakiwa na lengo kudumisha upendo na urafiki baina ya wachezaji na mashabiki wa mpira.
Akizungumza baada ya kukabidhi jezi hizo mara baada ya mchezo wa kwanza wa robo fainali, Mwenda alisema pamoja na kudumisha upendo na urafiki, mashindano hayo pia yamelenga kuwahamasisha vijana hao na wengine kuendelea 'kuchapa' kazi ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
" Michezo ni furaha, michezo ni upendo, nimefurahi kwa namna ambavyo nyote mlivyoonesha ushiriki mzuri wakati wote na zaidi mlivyonesha na kudumisha amani tangu kuanza kwa mashindano haya" alisema Mwenda
Aidha alisema mipango yake ni kuona Mikocheni inakuwa na timu bora ya mpira wa miguu ambayo itadhaminiwa na taasisi hiyo ya Mwenda ambayo hapo baadae itashiriki michuano mbalimbali ya ngazi zote hadi Ligi Kuu,.
Pamoja na hilo alisema kupitia timu hiyo matarajio ni kuona vipaji mbalimbali vya wachezaji vinapatikana na kutangazwa ili waweze kupata nafasi katika vilabu mbalimbali vya ligi za ndani na nje ya nchini.
Bingwa wa mashindano hayo atashinda zawadi ya Pikipiki huku mshindi wa pili akiibuka na kiasi cha Sh Milioni 1, mshindi Sh 500,000 na mshindi wa nne akiibuka na kifuta jasho cha Sh 250,000 huku fainali ya mashindano hayo ikitarajiwa kufanyika Desemba 25 mwaka huu.
Social Plugin