NEEC YAITUNUKU GGML TUZO YA MWEKEZAJI BORA KWA WATANZANIA


Makamu wa Rais wa GGML anayeshugulikia miradi endelevu, Simon Shayo (kulia) akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Being'i Issa (katikati). Tuzo hiyo imetolewa wiki iliyopita kwa GGML kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika kutekeleza vema muongozo wa'local content'.

Na Mwandishi wetu - Dar es salaam 

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limeitunuku Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) tuzo maalumu ya mwekezaji bora anayeshirikisha kikamilifu Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local content ) kwa mwaka 2021.

GGML ilikabidhiwa tuzo hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika kongamano la tatu la local content lililoandaliwa na Baraza hilo na kufanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa maktaba mpya uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akikabidhi tuzo hiyo kwa Makamu wa Rais wa GGML anayesimamia miradi endelevu, Simon Shayo, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Being’i Issa amesema GGML ni kampuni iliyotekeleza vyema muongozo wa Local Content na kuwa chachu kwa wadau wengine katika kuwezesha ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini.

Aidha, akifafanua sababu za kuipatia GGML tuzo hiyo, Katibu huyo wa NEEC alisema kampuni imeajiri wafanyakazi wengi zaidi ya 5000 ambao ni watanzania lakini vilevile katika menejimenti ya kampuni hiyo zaidi ya asilimia 90 ya viongozi wake ni watanzania wazawa.

“Pia imekuwa ikitekeleza program ya kuwajengea uwezo wananchi wa Geita wanaozunguka mgodi ili waweze kushiriki kazi mgodi huo.


“Kwenye mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR),kampuni ya GGML pia inaongoza kufanya vizuri tofauti na kampuni nyingine katika sekta ya madini.

“GGML pia inatekeleza program nyingine ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa Geita ili waweze kupata zabuni ndani ya Kampuni hiyo na kampuni nyingine. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo yametufanya tuone ni vema kuwatambua GGML,” alisema.


Alisema mbali na tuzo hiyo ya mwekezaji bora ambayo GGML ilipata, pia kuna tuzo ya kampuni bora ya kitanzania na tuzo ya wasimamizi bora wa miradi ambazo zote huandaliwa na NEEC na kutolewa kila mwaka.


Aidha, amesema lengo la kuipatia GGML tuzo hiyo pamoja na washindi wengine ni kuhamasisha kampuni zingine ziweze kuiga mfano wa GGML.

“Kwa sababu pamoja na kuwekeza, tunachoangalia ni uwekezaji wenye faida ndani ya jamii na taifa kwa ujumla. Pia tuzo zinalenga kuleta ushindani ili watu wafahamu kwamba ni jambo la muhimu kwa kampuni hizi kuunga mkono juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake.

“Lakini pia serikali inaweza kukutambua katika hilo eneo kwa sababu ukiangalia kwa mfano, GGML wanatoa fedha kwa Halmashauri za Geita zaidi ya bilioni 10 kila mwaka ambazo zinasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii, hivyo ni vyema kuwatambua,” amesema.

Aidha, Beng'i Issa alisema kongamano hilo linatoa fursa kwa watanzania kukuza uchumi jumuishi pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimkakati na utekelezaji wake.

Alisema utekelezaji wa local content nchini, umelenga kutoa ajira kwa watanzania, zabuni katika kampuni za kitanzania ikiwemo bidhaa wanazozalisha, mafunzo na uanzishwaji wa teknolojia pamoja na kuinua mfumo wa miradi.

Hata hivyo, alisema kongamano hilo linapanua ukuaji wa uchumi wa nchi ya Tanzania pamoja na kupanua wigo wa ajira kwa watanzania pamoja na kupunguza umaskini wa kipato.

“Local content imelenga kuzalisha ajira kwa wingi hususani kwa vijana ambapo ajira 52,000 zimeshazalishwa nchini kutokana na program ya local content ambapo asilimia 70 ni vijana kati ya umri wa miaka 20 mpaka 35,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post