Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NHC YATAKIWA KUTIMIZA AHADI RORYA


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dakt. Angelina Mabula akioneshwa ramani ya eneo la Saro plot na 400 wilayani Rorya mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo jana. Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Musoma Eliasa Keenja akimweleza jambo Naibu Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na ujumbe wake katika eneo la Saro plot no 400 wilayani Rorya alipokuwa katika ziara ya siku moja mkoa wa Mara.

*************************

Na Mwandishi Maalum, RORYA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dakta. Angelina Mabula (Mbunge), amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha katika mwaka ujao wa fedha linaanza kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa nyumba za makazi ishirini (20) katika eneo la Saro plot no 400 Wilayani Rorya Mkoani Tarime.

Dk. Mabula ameyasema jana katika kikao chake na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na Ofisi ya Kamishina wa Ardhi mkoa wa Mara.

Alisema kuwa, NHC ilitoa ahadi ya kujenga nyumba za makazi 20 katika eneo la Saro kwa ajili ya kupangishwa kwa watumishi wa Halmashauri na wananchi wengine, eneo liko tayari kwa ajili ya ujenzi huo na mahitaji ya nyumba ni makubwa sana.

“Nawaagiza NHC kuhakikisha katika kipindi kijacho cha mwaka wa fedha 2022/2023 mnaanza kutimiza ahadi yenu ya ujenzi wa nyumba hizo katika eneo hilo, kwani kiwanja tayari kipo na mahitaji ya nyumba ni makubwa kwani watumishi wa Halmshauri wanatoka maeneo ya mbali sana” Amesema Dk. Mabula

Aliongeza kwa kusema kuwa, kama NHC inashindwa kutimiza ahadi yake hiyo, basi fursa itolewe kwa taasisi zingine au makampuni ya ujenzi ambayo yatakuwa tayari kujenga nyumba hizo ambazo zitasaidia kupunguza adha ya makazi wanayoipata watendaji wa Halamashauri hiyo na kwa wananchi wengine ambao watahitaji kupanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Mahusiano NHC Muungano Saguya alisema kuwa, Shirika bado lina dhamira ya dhati kujenga nyumba 20 za makazi katika eneo la Saro kwa ajili ya kupunguza uhitaji wa makazi kwa watendaji wa Halmashauri, hivyo ahadi hiyo itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.

“Ni kweli NHC ilitoa ahadi ya ujenzi wa nyumba hizo na bado ahadi hiyo ipo, nikuahidi Mkuu wa Wilaya na watendaji wa Halmshauri muwe na subira, kwani Shirika haliwezi kuacha kuchangamkia fursa hiyo adhimu yenye lengo la kuisaidia Serikali kuhakikisha watendaji wake wanapata makazi bora” Amesema Saguya.

Kwa mujibu wa Saguya, NHC katika Mkoa wa Mara imejenga jengo kubwa na zuri la biashara la Mukendo Plaza katikati ya mji wa Musoma kwa ajili kupangisha lakini pia zimejengwa nyumba za makazi 50 eneo la Buhare ambazo zimepangishwa hivyo bado Shirika linaendelea na uwekezaji katika Mkoa wa Mara na mipango iliyopo ni kujenga jengo kubwa na biashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Kirongwe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com