Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza katika Mkutano wa wadau wa Nishati jadidifu na uzinduzi wa miradi ya Nishati jadidifu,uliofanyika jijini Dodoma Desemba 13,2021.
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Manfredo Fanti, akizungumza katika Mkutano wa wadau wa Nishati jadidifu na uzinduzi wa miradi ya Nishati jadidifu,uliofanyika jijini Dodoma Desemba 13,2021.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato(tatu-kulia) akikata utepe kuashiria kwa uzinduzi wa mradi wa Matumizi safi ya Nishati ya kupikia, uliofanyika jijini Dodoma Desemba 13,2021.
Picha za mtukio mbalimbali katika Mkutano wa wadau wa Nishati jadidifu na uzinduzi wa miradi ya Nishati jadidifu,uliofanyika jijini Dodoma Desemba 13, 2021.
**************
HAFSA OMAR, DODOMA
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema Serikali itahakikisha kuwa Nishati Jadidifu itakuwa moja ya chanzo kikubwa cha kuzalisha nishati nchini ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira nchini.
Ameyasema hayo, Desemba 13, 2021 wakati wa Mkutano wa wadau wa Nishati jadidifu na uzinduzi wa miradi ya Nishati jadidifu,uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua miradi hiyo ya nishati jadidifu, alisema kuwa nishati mbadala ni nishati ambayo inafaida kubwa ya kutochafua mazingira kwa upana wake na ina faida ya kutumika kidogo na kufanya kazi kubwa.
“ tumezindua miradi miwili, mradi wa kwanza unaofadhiliwa Umoja wa Ulaya lakini unapewa fedha na UN unalenga kuhakikisha kunakuwa na matumizi machache ya kuni na mkaa katika maeneo yetu, na mradi wa pili tuliozindua ni mradi unaolenga Zaidi kwenye kilimo lakini kwa kutumia umeme jua miradi yote hii imelenga katika matumizi sahihi ya nishati jadidifu”, alisema.
Alifafanua kuwa, mradi huo uliojikita kwenye matumizi ya Nishati safi ya kupikia, utaanza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza ambapo imeelezwa kuwa katika majiji hayo mkaa unatumika kwa kiwango cha juu kulinganisha na mikoa mengine, ambapo mkoa wa dar es salaam unaongoza kwa matumizi ya mkaa kwa asilimia 50 ya mkaa wote unaotumika nchini.
Sambamba na hilo, alisema Wizara imejipanga kuhakikisha kuwa mwaka huu inazalisha megawati 150 kutoka kwenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa maana ya jua na upepo na tayari Serikali imeanza kusaini mikataba na wawekezaji mbalimbali ili kuanza kutekeleza miradi hiyo.
Pia, Serikali imejipanga ifikapo mwaka 2025 kwa kutumia vyanzo mbalimbali ambavyo vipo nchini kuzalisha megawati 1100 zitokanazo na nishati jadidifu jambo ambalo litawezekana kwasababu kunampiango mizuri iliyopo na utekelezaji wake unaonekana.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Manfredo Fanti, alisema kuwa Mradi ambao umezinduliwa ni sehemu ya mashirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na Tanzania kwa upande wa sekta ya nishati.
Aidha, alisema mradi huo ni muhimu kwasababu utatoa mchango mkubwa katika kupunguza matumizi ya mkaa hasa katika maeneo ya mjini na vijijini.
Vilevile, amefafanua kwamba mradi huo hautasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira tu lakini pia utasaidia kuimarisha afya za watu kwakuwa hewa itokanayo na moshi wa matumizi ya mkaa na kuni unamadhara kwa afya ya mtumiaji