Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog-DODOMA.
JESHI la polisi nchini linawashikilia watuhumiwa 15 kutoka maeneo ya Dar es Salaam,Tabora,Mwanza na Tunduma kwa kosa la utengénezaji wa jezi feki jambo ambalo ni kosa la jinai linalo sababisha kukwepa kulipa kodi kutokana na kupitia kwenye mfumo usio rasmi.
Hayo yameelezwa leo na Msemaji wa Jeshi hilo Kamishna Msaidizi mwandamizi wa Jeshi la polisi(SACP) David Misime wakati akiongea na wananchi kupitia Vyombo vya Habari katika Ofisi za Makao makuu ya polisi Jijini Dodoma.
Amesema,katika msako ulioendeshwa na Jeshi hilo,zimekamatwa jumla ya jezi feki 279,urembo(ribons)300,na kofia 6 na kwamba kesi dhidi yao inaendelea .
"Kama mnavyo fahamu baadhi ya timu zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara huingia mikataba nankampuni mbalimbali za kutengeneza jezi na pale zinapouzwa kiasi fulani huingia katika timu ili kugharamia mahitaji ya wachezaji, lakini sasa kwa nia ovu watu wameanza kutengeneza na kuuza jezi zisizo na viwango ni kosa la jinai na hatutachoka kuwafuatilia,"amesema.
Pamoja na hayo amefafanua kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wamebainika kufanya mawasiliano na viwanda vya ndani na nje ya nchi ambavyo jezi halali hutengenezwa wakidai oda ya kutengenezewa jezi feki.
"Hawa nao jumla yao 11 tayari tumewafungulia jalada ,wamehojiwa na ushahidi unaendelea kukusanywa,"amesema.
Kutokana na hayo Misime ametoa wito Kwa watu wanaofanya hivyo kuacha mara moja kwani watachukuliwa hatua na kwamba timu zikibaini watu wanaotengeneza nembo za jezi tofauti na Mkataba walioingia na makampuni wasisite kutoa taarifa kituo chochote cha polisi .
"Tunawaomba mtambue jezi feki haziwafai,mnaumizwa kwa kuuziwa jezi zisizo na viwango kwa bei ileile ya jezi halali ambazo ukitumia hazidumu kama zile halali,tusilifumbie macho tatizo la bidhaa feki kwa sababi wahalifu wana tabia ya kunogewa wanaweza hata kuhamia katika kutibu binadamu wakati hawana utaalamu huo,"amesema Msemaji huyo wa polisi.