Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akishuhudia utiaji Saini Mkataba wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa Kilometa 368 katika kipande cha tatu cha mradi huo (Lot III). Wa kwanza (kushoto) ni Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli nchini (TRC) Bw. Masanja Kadogosa akiweka saini moja ya Kitabu cha Mkataba huo pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Yapi Merkez ya Uturuki Bw. Erdem Arioglu katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Desemba 2021.
Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli nchini Bw. Masanja Kadogosa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Yapi Merkez ya Uturuki Bw. Erdem Arioglu wakibadilishana Vitabu vya Mkataba wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa Kilometa 368 katika awamu ya tatu ya mradi huo (Lot III).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye Hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa Kilometa 368 katika kipande cha tatu cha mradi huo (Lot III) wa kwanza, hafla hiyo imefanyika leo tarehe 28 Desemba 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 28 Desemba, 2021 ameshuhudia utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha tatu kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368.
Utiaji Saini Mkataba huo umefanywa kati ya Serikali kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC) Bw. Masanja Kadogosa Pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Ujenzi ya Yapi Merkezi Bw. Erdem Arioglu kutoka Uturuki katika hafla iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa kipande hicho cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora utagharimu kiasi cha shilingi trilioni 4.41 ikujumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kufanya uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati ya vitano vya ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kufikia kiasi cha shilingi trilioni 14.7.
Mhe. Rais Samia amesema Serikali itahakikisha inaangalia namna yoyote na njia rahisi kwa ajilli ya kuchukua mikopo ya masharti nafuu itakayotufaa ili iweze kukamilisha miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Aidha, Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa fedha zinazokusanywa za tozo au kodi za ndani haziwezi kugharamia miradi mikubwa hivyo suala la kukopa litasaidia kumaliza hata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi huo wa Reli ya Kisasa kutoka Makutupora hadi Tabora.
Amesema kwa sasa Serikali imewekeza kiasi cha shilingi trilioni 14.7 hivyo tusipoendelea na ujenzi wa Miradi hiyo ya reli ya SGR fedha zilizokwishawekezwa zitakua hazina maana iwapo Serikali haitakopa ili kukamilisha miradi huo.
Mhe. Rais Samia amesema miradi yote mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere unaendelea vizuri na mpaka sasa Serikali haidaiwi fedha zozozte na Makandarasi katika miradi hiyo mikubwa.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Nchini (TRC) kukamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kipande kilichobaki cha Tabora hadi Isaka na kipande kipya cha Awamu ya Pili ya ujenzi wa reli ya SGR kutoka Tabora hadi Kigoma.
Mhe. Rais Samia amesema pia Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha kutoka sehemu ya Kaliua, Mpanda hadi Bandari kubwa ya Karema kuwa kiunganishi na bandari ya Kalemie kwa upande wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pia, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imepanga kujenga vipande vya reli vya kutoka Uvinza hadi Musongati (Burundi) na kuelekea hadi DRC, Isaka hadi Kigali (Rwanda), ambapo vipande hivyo vya reli vitajengwa kwa ushirikiano na nchi za Burundi, DRC na Rwanda ambapo kwa sasa mazungumzo ya namna ya kuchangia ujenzi yanaendelea.
Vile vile, Mhe. Rais Samia ameziomba Taasisi mbalimbali za fedha ulimwenguni kushiriki katika kugharamia ujenzi huo kwa kuwa utasaidia kuunganisha Tanzania na nchi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yao.
Mhe. Rais Samia amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya Tanzania kuweka misingi mizuri katika ukuaji wa uchumi wake kwasababu miundombinu ya reli na bandari itadumu kwa muda mrefu.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Social Plugin