**************************
NA NTEGHENJWA HOSSEAH-OR TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia Elimu), Gerald Mweli amesema, zaidi ya shilingi Bilioni 500 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili kuboresha Elimumsingi nchini.
Mheshimiwa Mweli ameyasema hayo leo Desemba 3,2021 katika ziara yake wilayani Kongwa mkaoni Dodoma.
"Fedha shilingi bilioni 304 kupitia mpango wa mapambano na ustawi wa jamii dhidi ya Uviko-19 zimepokewa ambapo Shilingi Bilioni 240 zinajenga vyumba vya madarasa 12,000
"Shilingi Bilioni 60 zinajenga vyumba vya madarasa 3,000 kwenye vituo shikizi 907 na Shilingi Bilioni 4 zinajenga mabweni 50 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum,"amesema Naibu Katibu Mkuu huyo anayeshughulikia Elimu.
Pia amesema, kupitia Programu ya GPE – LANES II na EP4R - Shilingi Bilioni 113 zimetolewa kujenga miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini.
"Kupitia programu hizo, ujenzi wa shule mpya za msingi 19 na sekondari 15 unafanyika kwa gharama ya shilingi Bilioni 21.25
"Fedha za tozo ya mawasiliano Shilingi bilioni 7 zimepelekwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya madarasa 560 ya shule za sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuunga mkono jitihada hizo.
"Vile vile fedha shilingi Bilioni 8.5 zimepokelewa kwa ajili kuzuia maambukizi na athari za UVIKO-19 zinajenga miundombinu ya kunawia mikono,"amebainisha Mheshimiwa Mweli.
Pia ameongeza kuwa, kupitia Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP) fedha shilingi Bilioni 130.5 zimetolewa kwa ajili ya kujenga shule 214 za sekondari za kata na shule 10 za wasichana za mikoa (shule moja kila mkoa) na hii ni katika mwaka huu wa fedha wa 2021/22.