RAIS Samia Suluhu Hassan siku ya Jumatano Desemba 15, 2021 anatarajiwa kufungua mkutano wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA), Titus Jumanne amesema mkutano huo utakaofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City unatarajiwa kuhudhuriwa na walimu 5,000 nchi nzima.
Amesema mkutano huo wa 16 unawaleta pamoja wakuu hao wa shule ili kubadilishana mawazo, uzoefu, changamoto, mafanikio na utekelezaji wa sera na mipango inayotolewa na serikali.
Amesema kwenye mkutano huo ambao unaratibiwa na global educatlon link kutakuwa na tukio la utoaji wa zawadi mbalimbali kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma.
Amesema mkutano huo utajadili mafanikio mbalimbali ya elimu yaliyopatikana katika awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi wa shule na maelfu ya madarasa mapya.
Pia ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha kwaajili ya ujenzi wa shule moja ya wasichana kwa mikoa 10 hali ambayo alisema itasaidia kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu watoto wa kike kwenda shule.
Amesema awamu ya sita imejitahidi kuhakikisha ufaulu kwenye elimu ya msingi na sekondari unaongezeka kwa kuweka miundombinu na walimu wa kutosha yote hayo ikiwa ni kuboresha elimu.
“Hiki ni kipindi cha kushangilia mafanikio ya elimu katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Rais wetu Samia atakutana na wakuu wa shule nchi nzima na kuzungumza nao masuala mbalimbali yanayohusu elimu na kuwapa mwelekeo wake kwenye sekta hiyo,” alisema Jumanne.
“Mkutano huu itakuwa fursa kubwa kwa walimu wakuu wa shule za sekondari kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali lengo ikiwa ni kuifanya sekta ya elimu iendelee kufanya vizuri,” alisema Jumanne.
Pia amemshukuru Rais Samia kwa kupeleka Sh bilioni 100 kwaajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya zipatazo 214 ambazo zitajengwa kwenye majimbo yote nchini ambapo Rais pia aliagiza Sh bilioni 30 zitumikekujenga shule mpya za wasichana pekee ambapo kwenye mikoa 10 itajengwa shule moja moja ya wasichana.
“Pia Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia imeagiza ujenzi wa shule za nsekondari 1,000 zitakazojengwa katika kata ambazo hazina shule za sekondari hii haijapata kutokea na serikali ya awamu ya sita inastahili pongezi za dhati kabisa,” amesema Jumanne
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo alithibitisha kuwa Rais Samia atakuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo wa walimu wa nchi nzima.