Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati ya ushauri ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa hafla iliyofanyika leo Desemba 16,2021 jijini Dodoma. Picha na Allex Sona
****
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua mpango kazi wa Taifa wa utekelezaji ahadi za Nchi kufikia kizazi chenye usawa ambayo ina jumla ya wajumbe 25 huku akieleza azma yake ya kutenganisha Wizara ya afya na kuitenga wizara itakayoshughulikia Jinsia na maendeleo ya wanawake na mambo mengine.
Akizindua mpango huo mapema leo Desemba 16,2021 Jijini Dodoma ,amesema kuwa utasaidia Tanzania kuendelea kuwa kinara katika mataifa ya Afrika kwa kuhakikisha usawa wa mwanamke kumiliki mali unatekelezwa ipasavyo.
Rais Samia amesema,"lakini kama tutatenga vipengele vingine vilivyobaki na afya tukaisimamisha ikabaki peke yake usimamizi wa sera,sheria ,na mambo mengine unaweza kwenda vizuri na kupata msukumo unaohitajika,kwa hiyo hayo ndiyo maamuzi yangu na nitajaribu kumshawishi Rais wa Zanzibar naye afanye hivyo,"amesema.
Amesema hatua hiyo itasaidia kutoka kwenye kuchanganywa na wizara ya afya na kwamba Wizara hiyo ina mambo mengi ukilinganisha na hali ilivyo sasa duniani sekta ya afya peke yake inachukua sura kubwa ya wizara hiyo kuliko vipengele vingine vilivyobaki.
Akizungumzia uzinduzi huo amesema kuwa nusu ya watu duniani ni wanawawe na iwapo wanaweza kutumiwa vizuri wanaweza kuzalisha Dola Trilioni 28 kwa mwaka .
Amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa makubaliano ya mkutano wa Beijing Nchini China lakini bado mataifa mengi hayajatoa kipaumbele kwa wanawake katika nyanja mbalimbali na kusababisha wasifikie kiwango kinachotakiwa cha uzalishaji.
"Pamoja na malengo yaliyowekwa lakini bado malengo hayajafikiwa kwa kiwango kinachotakiwa hivyo kuna kila sababu ya kufikia malengo na yatafikiwa hasa kwa kutumia kamati ambayo umeteuliwa" ameeleza Samia.
Aidha ameziagiza sekta zote za serikali kuhakikisha zinatenga bajeti na kutoa kipaumbele kwa kuendeleza na kufanikisha suala la kizazi cha usawa ambacho ni kwa kipindi cha miaka mitano.
Sambamba na hilo amesema wastawi wa Jamii wawezeshwe ili waweze kutekeleza majukumu yao nchini ikiwa ni kufanikisha pamoja na mataifa mengine na balozi zilizopo Tanzania kuunga mkono jambo hilo.
Katika hatua nyingine Rais Samia ametoa maagizo kwa Kamati kuwa ni lazima kutoa ushauri bora na wa kimkakati,kushauri namna bora mpango kazi kwa kujumuisha wadau na mamlaka ya nchi na kutoa elimu ya kujenga usawa.
Agizo lingine ni kuhakikisha usawa unajengewa mazingira mazuri sambamba na kuona namna ya kuwezesha vizuri uchumi wa jamii.
Aidha amesema anatarajia kuigawa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto na kuunda wizara ya maendeleo ya jamii ili kutoa msukumo katika utekelezaji wa mipango na sera za masuala ya usawa wa kijinsia.
Amesema anaelewa kuwa wizara hizo mbili zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu ikiwa ni pamoja na maandalizi ya tukio hilo.
“Sasa ndugu zangu unaweza kuona kwamba pamoja na jitihada zote tulizozifanya na sera zote tulizoweka lakini bado hatujafika tulipotakiwa kufika.
"Sasa ili tuweze kufika tunapotakiwa kufika, ni lazima kuwe na usimamizi, uratibu, utathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wetu wa mipango.
“Kwa hiyo hayo ndiyo maamuzi na ninatajaribu kumshawishi Rais wa Zanzibar ili naye afanye vivyo hivyo ili tuende vizuri,” amesema.
Aidha aemsema baada ya miaka 20 tangu kutolewa kwa azimio la Beijing la kumkomboa mwanamke, bado serikali nyingi duniani zimeshindwa kutekeleza sera za kumuinua mwanamke kiuchumi.
Amesema kumekuwa na vikwazo vingi katika maeneo ya afya, elimu, mila kandamizi, upatikanaji wa mitaji, teknolojia inayoweza kuwarahisishia kazi zao, masoko, huduma za ugani, hifadhi ya jamii na unyanyasaji wa aina mbalimbali.
Naye Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk. Dorothy Gwajima amesema kuwa wamekuwa wakiimarisha na kuharakisha shughuli katika jukwaa la matokeo ya Beijing kwa miaka 25 sasa.
Social Plugin