Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YAREJESHA DARASA LA SABA KWENYE MFUMO WA ELIMU


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza kurejesha rasmi darasa la saba katika mfumo wa elimu ya msingi.

 Sera ya elimu ya mwaka 2006 inaelekeza elimu ya Msingi ya miaka sita kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la sita.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said amesema leo Ijumaa Desemba 24, 2021 kwamba lengo la kuishia darasa la sita ilikuwa ni kumuwezesha mwanafunzi kupata fursa za elimu ya maandalizi, msingi na sekondari akiwa na umri mdogo.

“Kutokana na mabadiliko mbalimbali na mikakati ya maendeleo nchini pamoja na changamoto tofauti zinazoikabili sekta ya elimu, Wizara imeona ipo haja ya kufanya tathmini kwa kina na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo.

“Wizara pia imepanga kufanya mabadiliko katika ngazi ya elimu ya msingi kwa kurejesha darasa la saba, kwahiyo mabadiliko haya yataifanya elimu kuwa ya darasa la saba kuanzia mwaka wa elimu 2022,” amesema

Amesema mahitaji yote ya msingi ikiwemo mitaala, walimu, vitabu na madarasa vimezingatiwa na kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuanza darasa hilo.

Kuhusu walimu, alisema wizara imefanya tathmini na kuona kuwa walimu waliopo katika ngazi ya maandalizi na msingi wanatosheleza kufundisha katika ngazi hiyo likiwemo darasa la saba.

Kuhusu vitabu, Simai alisema vilivyopo sasa pia vinaweza kutumika kwa kuanzia wakati wizara inatayarisha vitabu vipya kwa madai hakutokuwa na mabadiliko makubwa ya mada zinazopaswa kusomesha elimu ya msingi, ila mabadiliko yanaweza kutokea kwa mada na darasa husika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com