Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akiongea na vyombo vya habari kuhusu ziara aliyoifanya na kuonyeshwa kuridhshwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
***
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog, DODOMA.
KAMATI ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma imetembelea na kukagua ujenzi wa vyumba vya Madarasa yanayojengwa kwa kutumia fedha za Uviko 19 huku ikiagiza ujenzi huo kuendana na utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa wingi na kuepuka kuchimba ovyo madini ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ametoa maelekezo hayo leo mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ambapo wamekagua vyumba vya madarasa katika Shule za Sekondari za Miyuji,Umonga,Kiwanja cha ndege,Viwandani,Itega na Dodoma Sekondari ikiwa ni pamoja na kukagua karakana zinazotengeneza Madawati.
Mtaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma ameonyesha kuridhishwa na Ujenzi wa madarasa hayo huku akisema ni vyema ujenzi wa vyumba hivyo vya Madarasa ukazingatia suala zima la upandaji miti katika utunzaji wa Mazingira.
"Sasa nipende kuwaagiza kuwa lazima ujenzi huu uendane na thamani ya pesa kama Mheshimiwa Rais ambavyo amekuwa akisisitiza kila siku lengo hapa ni kuona watoto wetu wananufaika na miradi hii,"amesema.
Katika hatua nyingine,Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi na walenzi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha ifikapo Januari 17 Mwaka 2022 watoto wote wawepo shuleni.
"Hili sio ombi nasisitiza kwa jinsi Mradi wa ujenzi wa vyumba hivi vya Madarasa unavyoendelea mmenihakikishia mmefikia asilimia tisini ya ujenzi nataka tarehe hiyo 17 Januari watoto wote waripoti shuleni ili wapate haki ya msingi kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla,"amesisitiza.
Hata hivyo ameutaka Uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanakamilisha Ujenzi huo wa vyumba vya Madarasa kwa wakati ili watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato Cha kwanza waweze kusoma.
Naye Katibu tawala mkoa wa Dodoma Fatma Mganga amesema Dodoma ilikuwa na upungufu wa madarasa ya sekondari 601 huku akisema wanatarajia kupokea wanafunzi 10,755 kidato cha kwanza 2022 Mwaka huu.
Awali Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Joseph Mafuru ameihakikishia Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dodoma kuwa hadi ifikapo Disemba 24 Mwaka huu watakabidhi Madarasa hayo.
"Sisi kama Jiji tunajitahidi katika kutekeleza Mradi huuu na tunamshukuru Sana mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa watoto ambao walikuwa wanakosa nafasi kuweza kusoma,"amesema
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Fredrick Mwakisambwe akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa 147 yanayotekelezwa kupitia Mradi huo wa uviko 19 katika Halmashauri hiyo amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya juhudi kubwa ya utekelezaji wa miradi hiyo.
"Miradi hii inafanyika kwa kuzingatia kiwango cha ubora yaani thamani ya Fedha ambapo ujenzi huo unaenda sambamba na utengenezaji wa Madawati,"amesema.
Ikumbukwe kuwa Serikali ya Tanzania hivi karibuni ilipokea kiasi Cha Shilingi Trilioni1.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo toka Shirika la Fedha Duniani IMF ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alielekeza matumizi ya fedha hizo kwenye shughuli mbalimbali za Maendeleo nchini.
Social Plugin