Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA IKO MBIONI KUANZA UZALISHAJI WA MKAA MBADALA WA MAKAA YA MAWE KWA MAJUMIZI YA NYUMBANI


NA: Hughes Dugilo, ZANZIBAR.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Vennance Mwasse amesema kuwa Shirika hilo lipo kwenye hatua za mwisho za kupokea mashine maalum itakayotumika kutengeneza mkaa mbadala wa makaa ya mawe (Rafiki Briquettes) ili mkaa huo uweze kutumika majumbani.

Dkt. Mwasse ameyasema hayo Disemba 7,2021 katika Maonesho ya Sekta ya Viwanda yanayoendelea kwenye viwanja vya Maisala Mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na wadau mbalimbali waliofika kwenye Banda la STAMICO kujionea na kijifunza namna mkaa huo unavyozalishwa.

Aidha amesema kuwa maandalizi ya kutengeneza mkaa huo  mbadala yamekamilika nakwamba kinachosubiriwa ni Mashine hiyo itakayotumika kutengeneza maumbo ya mkaa huo  na kuanza kutumika majumbani.

“Mpaka sasa kila kitu kipo tayari tunaisubiri mashine maalum itakayotumika kutengeneza mkaa huo mwezi huu wa Disemba na baada ya hapo utaanza kuuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu ili kuanza kutumika majumbani” Amesema Dkt. Mwasse.

Akijibu swali la moja ya wana habari aliyehoji juu ya kuwepo uwezekano wa mkaa huo kupatikana Visiwani Zanzibar, Dkt. Mwasse amefafanua kuwa “Mara Baada ya kuanza uzalishaji rasmi tutaweka utaratibu mzuri wa kibiashara wa kuusambaza mkaa huu nchi nzima ikiwemo hapa Zanzibar kwa kutumia mawakala watakaojitokeza kufanya kazi hii lengo letu ni kuhakikisha kila mtanzani anapata Bidhaa hii na kufurahia rasilimali zao” Amefafanua.

Aidha amepongeza maandalizi ya maonesho hayo nakwamba imekuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho hayo kufanyika Zanzibar hivyo imetoa fursa kubwa kwao kama STAMICO kuweza kukutana na wananchi wa Visiwa hivyo ili nao wapate elimu na kuweza kufahamu shughuli mbalimbali za Shirika hilo.

Mapema baada ya kuwasili viwanjani hapo Dkt. Mwasse alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda kujionea shughuli mbalimbali za Taasisi zilizoshiriki Maonesho hayo ambapo pia aliweza kujumuika na wananchi wengine katika siku maalum ya kula Korosho iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Maonesho hayo yanayoendelea Mjini Zanzibar yenye kaulimbiu isemayo “MIAKA 60 TANZANIA IMARA KAZI INDELEE” yanafikia kilele chake Disemba 9 Mwaka huu yakienda sambamba na Shamrashara za kumbukizi ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika ambapo kilele chake ni tarehe 9 Disemba, 2021.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com