Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

100 WAPATA AJIRA UWANJA UNAOJENGWA NA GGML GEITA


ZAIDI ya Watanzani 100 wamepata ajira katika mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo unaojengwa katika mtaa wa Magogo halmashauri ya Mji Geita mkoani Geita kwa ufadhili wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).

Katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja huo, jumla ya shilingi bilioni 2.4 zinatumika kupitia fedha mfuko wa Uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) zinazotolewa na kampuni hiyo.


Akielezea mwenendo wa ujenzi huo hivi karibuni Mjini Geita, Mhandisi ujenzi katika Mradi huo, Lt. Kanali Samuel Hagu alisema mradi huo unatekelezwa kwa ubia baina ya GGML na Halmashauri ya mji Geita.


Alitolea mfano kuwa maandalizi ya bajeti ya ujenzi ambayo ni Sh bilioni 2.4 na usanifu wa mradi huo, vyote vimefanywa na halmashauri ya mji Geita kwa kushirikiana na GGML.

“Awamu ya kwanza ya mradi wetu ilianza kutekelezwa tarehe 16 Julai, 2021,matarajio yalikuwa kutekeleza kwa miezi minne lakini bado tunaendelea kukamilisha baadhi ya vitu,”alisema.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu zinazolenga kunufaisha jamii ya mji wa Geita, walishaurina na kampuni ya GGML mambo mbalimbali kuleta tija na matunda yanayotarajiwa katika Mradi huo.

“Tulikubaliana kuleta wafanyakazi karibia 50 kutoka kwenye kampuni zinazotekeleza Mradi huu lakini tukachukua nusu iliyobakia ya Wafanyakazi kutoka kwenye jamii ya mji wa Geita.Kwa hiyo tuna wafanyakazi zaidi ya 100, pia kuna huduma mbalimbali ambazo zinawanufaisha wananchi wanaozunguka mradi kama vile mama lishe,”alisema.


“Kwa hiyo wananufaikaji wa moja kwa moja kupitia utekelezaji wa mradi ndio hao lakini baadae kutakuwa na wanufaikaji wengine kupitia uingizaji wa watu wakati uwanja utakapoanza kutumika,”alisema.


Aidha, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo amesema kampuni hiyo itaendelea kuzishirikisha kikamilifu Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Geita katika miradi yote inayotekelezwa kupitia fedha za mfuko wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Alisema GGML ina makubaliano ambayo waliingia pamoja na Halmashauri hizo mbili ya kuwa kila mwaka watatoa Sh bilioni 9.2 kwa ajili ya huduma za kijamii.

“Kamati ya Uwajibika wa Kampuni kwa Jamii (CSR) yenye wajumbe kutoka halmashauri hizo pamoja na kampuni ya GGML hukaa pamoja kisha GGML wanapendekeza miradi ambayo hujadiliwa kwa pamoja na kutekelezwa kwa ushirikiano.

“Kwa hiyo hata katika ujenzi wa uwanja huu mathalani halmashauri imemtafuta mkandarasi na GGML imetoa fedha za kutekeleza mradi huo,” alisema.

Halmashauri ya Mji wa Geita ilitenga eneo lenye hekta 10.4 kwa ajili ya kujenga uwanja huo wa kisasa wa michezo ambao ndani yake kutakuwa na kiwanja cha mpira wa miguu, njia za mchezo wa riadha, maeneo ya biashara na maegesho ya magari.

Uwanja huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 12,000 wote wakiwa wameketi.

Katika awamu ya kwanza ya ujenzi miundombinu muhimu inayojengwa ni pamoja na Jukwaa kuu, kiwanja cha mpira wa miguu, vyumba vya wachezaji, chumba cha waamuzi, chumba cha kupima wachezaji, chumba cha huduma ya kwanza, Ofisi ya meneja wa uwanja na chumba cha mikutano.

Vilevile unajengwa uzio wa ukuta wa tofali na milango ya kuingilia na uchimbaji wa kisima kirefu cha maji na matanki ya kuhifadhi maji kwa ajili ya ujenzi na matumizi ya uwanja.
Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ukiendelea katika mtaa wa Magogo katika halmashauri ya Mji Geita mkoani Geita kwa ufadhili wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com