JESHI la Polisi nchini Nigeria wanasema wanaendelea kuchunguza tukio la vifo vya watoto nane wa familia mbili tofauti, waliokutwa wamekufa ndani ya gari katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos.
Watoto hao wa kiume, wenye umri wa kati ya miaka minne hadi sita, walikutwa wakiwa wamekufa ndani ya gari mwishoni mwa wiki iliyopita, huku gari hilo likiwa limetelekezwa na bado haijabainika jinsi walivyofungiwa katika gari hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi katika Jimbo la Lagos, miili ya watoto hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini sababu halisi ya vifo vyao.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa kamishna wa polisi wa jimbo hilo, Hakeem Odumosu, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa haraka kuhusu tukio hilo.
Wazazi wa watoto hao, wanasemekana kuwa raia wa Niger wanaoishi Lagos ambapo mwenyekiti wa Waniger wanaoishi Lagos, Saidu Abdullahi, ameliambia Shirika la Habari (BBC) kuwa wanaomba mamlaka husika zifanye uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya vifo vya watoto hao.
Social Plugin