Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUANZA KUPANDIKIZA MIMBA KWA WANAWAKE WENYE MATATIZO YA UZAZI



ZIKIWA zimebaki siku chache kufunga mwaka wa 2021, ndoto ya Tanzania kuanza kutoa huduma ya kupandikiza mimba kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi imeanza kuonekana kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Hospitali hiyo ilianzishwa 2015 kwa tamko la Rais wa nne, Jakaya Kikwete na ilizinduliwa rasmi Oktoba 13, 2015 na imefanikiwa kuwa hospitali yenye huduma zote za kibingwa na baadhi ya huduma za ubingwa bobevu ikiwamo kupandikiza figo.

Hospitali hiyo sasa imeanza kupandikiza mimba kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi.

Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika katika taarifa yake wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wakurugenzi wa hospitali hiyo agusia maendeleo waliyofikia

“Menejimenti imekusudia kuanzisha huduma nyingine za ubingwa bobevu kama vile upandikizaji wa uroto (Bone Marrow Transplant), upandikizaji wa mimba (IVF) na matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi.”

Hata hivyo, kauli yake hiyo ilifafanuliwa zaidi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Dk Dorothy Gwajima aliyesema amekuwa akisumbuliwa kwa kupigiwa simu nyingi na wanawake wenye matatizo ya uzazi wakitaka kujua namna Serikali itakavyosaidia kuondoa tatizo hilo.

“Nimekuwa nikipigiwa simu nyingi na wenye matatizo ya uzazi kwa kuwa gharama za kupandikiza mimba kwenye hospitali binafsi gharama zake ziko juu.

“Anna uko wapi hebu njoo hapa,” Dk Gwajima alimuita Dk Anna Kasililika ambaye ni daktari wa mifumo ya uzazi anayeshughulikia kitengo cha matibabu ya uzazi ili atoe maelezo kwenye hadhara iliyofanyika kwenye eneo la Hospitali ya Benjamin Mkapa katikati ya Novemba, 2021.

Kuonyesha kwamba mwaka 2021 unaisha kwa matumaini na mwaka ujao unaanza kwa mafanikio, Dk Kasililika aliyesomea utaalamu huo kutoka Chuo Kikuu cha Pan African cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika mwaka 2019, anasema waliishaanza majaribio, lakini wanatarajia kuanza rasmi Januari mwakani.

“Tulianza kupandikiza mimba kwa mtu mmoja, lakini bahati mbaya ujauzito ulitoka,” alisema Dk Kasililika.

Anna anasema wanachofanya ni kupandikiza mbegu za kiume kwenda kwenye kizazi cha mwanamke mwenye matatizo ya uzazi. Hata hivyo, Dk Chandika anasema maandalizi ya vitanda 400 kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ya upandikizaji mimba yameanza na Januari, 2022 yatakuwa yamekamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com