Shughuli katika mji wa Embu zilisimama kwa muda baada ya mwanamume aliyekuwa uchi anayeaminika kuwa mlevi kuiba gari na kutoweka nalo.
Mwanamume huyo anasemekana kuiba gari hilo kutoka kwa jamaa mwingine katika eneo la Kamuketha katika mji wa Embu kabla ya kuliendesha .
Hata hivyo, haijabainika ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alifanikiwa kupata funguo za gari hilo kabla ya kuondoka nalo.
Baada ya kuponyoka, mmiliki wa gari hilo aliwarai wahudumu wa bodaboda kulifuata gari hilo.
Mwanamume huyo alipogundua kuwa anafuatwa, aliendesha gari hilo hadi kwenye maegesho ya maduka makubwa katika mji wa Embu kisha akaruka nje.
Mlinzi aliyekuwa akisimamia eneo la maegesho hayo alijionea maajabu na alipomuuliza jamaa kilichokuwa kikiendelea alimgeukia akamzaba kofi na mateke.
"Gari liliendeshwa kwa kasi hadi kwenye eneo la maegesho lakini hatukujua kilichokuwa kikifanyika hadi tulipofahamishwa kuwa gari hilo lilikuwa limeibiwa," jamaa aliyetambulika kama Evans Mong'are ambaye alishuhudia kisa hicho aliambia K24 Digital.
Mlinzi wa eneo hilo alipiga kamsa kuitisha msaada na kwa bahati nzuri wahudumu wa boda boda walikuwa wamefika.
Wanabodaboda hao walijaribu kumnasa jamaa huyo aliyekuwa uchi lakini aliwashambulia kwa mawe huku akijaribu kuhepa.
Hata hivyo wahudumu hao walijitahidi na hatimaye wakafanikiwa kumnasa jamaa kisha wakamkabidhi kwa polisi.
Magari kadhaa yalihabiriwa wakati wa tukio hilo. Mwanaume huyo alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Embu huku maafisa katika kituo hicho wakiahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu kesi yake.
"Nitathibitisha maelezo zaidi kuhusu tukio hilo baada ya kupokea taarifa zaidi kutoka kwa maafisa niliowatuma katika eneo la tukio," Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Embu Magharibi Julius Kyumbule alidokeza.
Via - Tuko News
Social Plugin