Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Enos Kadange baada ya kuagwa nyumbani kwake Kichangani Mpanda ukisubiri kusafirishwa kwenda Buhoro Kasulu kufanyiwa maziko.
***
Mchungaji wa kanisa la FPCT Mpandahoteli Manispaa ya Mpanda Enos Kadange (53) amefariki dunia baada ya kugongwa na basi wakati akiendesha pikipiki kuwahi ibada.
Ajali hiyo imetokea Januari 1, 2022 maeneo ya Super City kata ya Majengo makutano ya barabara ya Mpanda-Sumbawanga ikihusisha pikipiki basi hilo linalofanya safari zake Mpanda-Karema.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 4, 2021 Askofu wa makanisa ya Kipentekost jimbo jipya la FPCT Mkoa wa Katavi, Julias Lumela amesema wamepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa msiba huo.
Amesema mchungaji huyo alipata ajali wakati akiwahi ibada na kwamba alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu hospitali ya rufaa Mkoa wa Katavi.
“Aliagana vizuri na mke wake baada ya kufika eneo hilo alipata ajali, aliburuzwa madaktari walidai amevuja damu nyingi na ilivujia kwenye ubongo na baadhi ya viungo vya mwili vilivunjika,” amesema Lumela.
“Wasamaria wema walimuokota na walimpeleka hospitali lakini alipoteza maisha, ametumikia maisha ya uchungaji zaidi ya miaka 10,”
“Hatujui siku wala saa tutakayopatwa na mauti, mfano Mchungaji wetu wazo lake lilikuwa kwenda kuendesha ibada lakini ghafla jambo likajitokeza asilolitegemea hakuna aliyelipanga,”
Mdogo wa marehemu na mkazi wa Kakese, Alfred Kadangi amesema walipokea taarifa za kifo hicho cha ndugu yao wakiwa kwenye ibada.
Hamis Misigalo mzee wa kanisa la FPCT Mpanda mjini amesema marehemu alikuwa mkarimu alimfahamu wakati akiwa mwinjilisti wa kanisa hilo, baadaye alihamishiwa Mpandahoteli.
“Alikuwa mtu mzuri hana shida tumepata pengo kubwa waumini na sisi viongozi wenzake imetuumiza sana Mungu ndiye aliyeamua amemtwaa,” amesema Misigalo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amethibitisha kutokea tukio hilo akidai kuwa dereva wa basi hilo Isaya Leonard mkazi wa Kigamboni anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva pikipiki kuingia barabara kuu bila kuchukua tahadhari, alisafirishwa jana kwenda Buhoro Kasulu kwaajili ya maziko,” amesema Makame.
CHANZO - MWANANCHI
Social Plugin