Watu 14 wamepoteza maisha wakiwemo wanahabari watano na abiria wa kawaida katika ajali iliyohusisha magari mawili ikiwa moja ni la abiria aina ya Toyota Hiace na jingine lenye namba za usajili STK 8140 mali ya Serikali lililokuwa limebeba waandishi wa habari mkoa wa Mwanza wakitokea Mwanza kuelekea Ukerewe kupitia Bunda, Mara kugongana uso kwa uso leo Jumanne 11, 2022.
Gari la waandishi wa habari lililokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel limegongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Busega (DC), Gabriel Zakaria amesema kati ya vifo hivyo kuna vifo vya waandishi wa habari wanne na dereva wa waandishi na watu wengine sita walifariki papo hapo.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea, watu 11 wamefariki kwenye eneo la tukio wakiwemo waandishi wa habari wanne na dereva na wengine sita waliokuwa kwenye gari lingine. Dakika chache majeruhi waliopelekwa kwenye kituo cha afya cha Nasa watatu walifariki, wakiwemo wale waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara”, amesema
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyo, Blasius Chatanda amesema yupo katika hospitali ambako majeruhi walikopelekwa akiahidi kuwa atatoa taarifa baadaye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Bw. Emmanuel Luponya Sherembi, ameahirisha ghafla ratiba ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi Robert Gabriel kwa ajili ya kukabidhi miradi baada ya ajali iliyotokea saa chache na kusababisha vifo.
"Mkurugenzi Mtendaji anasikitika kuwafahamisha kuwa, ratiba ya ziara ya leo ya kukabidhi miradi yetu kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeahirishwa ghafla.
"Hii ni kutokana na ajali mbaya iliyoukumba msafara wa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wakati akiwa anakuja ambapo gari lilokuwa limebeba kikosi cha waandishi wa habari limegongana na Hiace uso kwa uso maeneo ya Busega.
"Taarifa zinasema kuwa watu watano wamepoteza maisha ambao inasemekana kuwa ni waandishi na maafisa habari ndani ya mkoa wetu na pia inasemekana kuwa mojawapo ya waliofariki ni pamoja na ofisa habari na mahusiano wetu, Bw.Stephen Msengi.
"Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa na kuthibitishwa. Kufuatia hali hiyo, uongozi wa mkoa na wilaya umeamua kusitisha ratiba ya ziara hii hadi siki nyingine itakayopangwa.Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amen"
Taarifa za awali zilizotolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko imeeleza kuwa tukio hilo limetokea katika Wilaya ya Busega, Simiyu na kwamba waandishi wa habari watano wamepoteza maisha katika ajali hiyo.
Taarifa za awali
Gari la waandishi wetu wa Mkoa wa Mwanza lililokuwa kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza limepata ajali eneo la Busega lilikuwa linaelekea Ukerewe kwa kupitia Bunda.
Nineongea na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ng. Gabriel amethibitisha kutokea taarifa za watu watano waliokuwa kwenye gari hilo lililobeba waandishi kufariki dunia.
Majina ya wenzetu hao tutayatoa kadri tutakavyofuatilia. Kwa sasa Mkuu wa Mkoa nae anaelekea eneo la tukio nasi pia tunajipanga kwenda eneo la tukio.
Naomba tuwe watulivu kwa wakati huu, wakati team yetu na ya Mkuu wa Mkoa tunafuatilia tukio hilo.
Edwin Soko
Mwenyekiti
Mwanza Press Club
11.01.2022.