Waswahili wanasema Mungu akitaka kukupa hakuandikii barua! Usemi huo unaonekana kutimia kwa mzee Jemba Matte, mkazi wa Kyerima, Kayunga nchini Uganda ambaye hivi karibuni amejizolea umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Sababu kubwa iliyomfanya mzee huyo a-trend kwenye mitandao ya kijamii, ni kusambaa kwa picha yake akiwa anasoma tangazo msibani, ambapo anaonekana mkono mmoja akiwa ameshika kipaza sauti huku mkono mwingine akiwa na rundo la karatasi ambazo hazijapangiliwa vizuri.
Picha hiyo ilianza kusambaa mitandaoni kama masihara, watu wengi wakawa wanaitumia kama ‘meme’ na kuwafanya wengi wawe wanacheka na kuvutiwa nayo wanapokutana nayo mitandaoni.
Ni hapo ndipo baadhi ya vyombo vya habari nchini humo, vilipoanza kumtafuta mzee huyo kwa lengo la kujua undani wa maisha yake na mengi kuhusu picha hiyo ambayo tayari ilishakuwa gumzo ndani na nje ya Uganda, ikiwemo hapa nchini na nchi jirani ya Kenya.
Baada ya mzee Jemba kupatikana, ndipo alipoeleza kwamba kumbe picha hiyo, ilipigwa akiwa anasoma wasifu wa marehemu msibani, kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa miaka mingi, tena kwa uzoefu wa hali ya juu.
Baada ya mahojiano yake kusambaa, wengi walizidi kuvutiwa na mzee huyo kutokana na mbwembwe zake anapokuwa anasoma matangazo msibani na kwa kuwa alieleza kwamba anaishi maisha duni, akijishughulisha na kilimo huku mkewe waliyezaa naye watoto 11 akimkimbia, wasamaria wema walianza kujitokeza kumsaidia.
Miongoni mwa misaada ya awali aliyoipata, ilikuwa ni fedha, simu na redio kwa ajili ya kumrahisishia kazi yake ya kusoma wasifu wa marehemu kwenye misiba, ambapo alieleza kwamba huwa anaifanya kazi hiyo bure na wafiwa humpoza kwa chochote wanachokuwa nacho.
Maisha yake yakaanza kubadilika, misaada ikazidi kumiminika, baadhi ya wasanii akiwemo Boby Wine ambaye pia ni mwanasiasa, naye akatoa msaada kwa mzee huyo, akieleza kwamba amewahi kumshuhudia katika moja ya misiba, akifanya kazi yake!
Msanii mwingine chipukizi, Gravity Omutujju naye akaamua kumtumia mzee Jemba kwenye video yake, ambapo anaonekana akisoma matangazo katika video ya wimbo huo, akalipwa chake na maisha yakazidi kumnyookea.
Habari mpya ambazo zinazidi kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ni kwamba baada ya kuishi kwa upweke kwa takribani miaka mitatu tangu mkewe amkimbie, mzee amepata zari la mentali kwa kupendwa na binti mrembo mwenye fedha zake.
Picha za wawili hao wakila bata kwenye hoteli ya kitalii ya Freedom City Sauna, Gym and Pool zimezidi kuufanya umaarufu wa mzee huyo kuongezeka maradufu, wengi wakimpongeza kwa kuopoa kifaa kama hicho katika umri wake mkubwa!
Haijafahamika bado mrembo huyo ni nani ingawa mitandaoni anatumia jina la Sexy Mbu, lakini picha hizo zinawaonesha wakiwa kwenye mahaba mazito na kuzidi kuwafurahisha wengi mitandaoni huku mwenyewe akidai kwamba hajampendea babu umaarufu wala fedha, bali ni mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake!
Huyo ndiyo mzee Jemba aliyetrend kwenye mitandao, ambaye sasa anafaidi penzi la msichana mrembo na kuzidi kuzua gumzo kwenye mitandao ya kijamii!
Social Plugin