CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza mchakato wa kumsaka mrithi wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ambaye alijiuzulu tarehe 6 Januari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 9 Januari, 2022 Visiwani Zanzibar, Katibu wa NEC- Itikadi Uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka amesema mchakato huo utaanza kuanzia tarehe 10 hadi 30 Januari mwaka huu.
Amesema hatua hiyo imekuja baada ya Ndugai kuandika barua kwa hiari yake na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma.
Amesema kufuatia hilo CCM kinawatangazia wanachama wake wote kwamba utaratibu wa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea atakayechaguliwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujaza nafasi ys Spika wa Bunge.
Amesema utaratibu huo ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayotambua Spika kuwa ndio kiongozi mkuu wa Bunge na nafasi hiyo haiwezi kuwa wazi na Bunge likaendelea kufanya shughuli zake.
Akinukuu Katiba hiyo amesema; Ibara ya 84 (i) kutakuwa na Spika ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge, atakuwa ndio kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge.
“Ibara ya 84(viii) inasema hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa katika Bunge isipokuwa uchaguzi wa spika wakati wowote ambao kiti cha spika kipo wazi.
“Ibara ya 86(i) kimeeleza kutakuwa na uchaguzi wa spika katika kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya, na katika kikao cha kwanza chochote mara baada ya kutokea kiti cha spika kuwa wazi.
“Kwa minajili hiyo, katika kutekeleza matakwa ya kikatiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, nichukue fursa hii kwa niaba ya chama kutangaza kwamba mchakato wa kujaza kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utatekelezwa kwa ratiba ifuatayo sambamba na vikao vya mchujo na uchaguzi wa wabunge wa CCM kabla ya kupelekwa bungeni kuendelea na utaratibu mwingine,” amesema.
Amesema kuanzia tarehe 10 hadi 15 zoezi la kuchukua fomu litaanza rasmi na tarehe 15 ifikapo alasiri zoezi hilo litakuwa limekamilika.
Amesema wale wenye sifa alizotaja wanakaribishwa kuchukua fomu katika makao makuu ya chama ofisi kuu, makao ya chama Dodom, ofisi ndogo Dar au Kisiwandui wakifika watapata maelekezo namna ya kcuhukua fomu hizo.
Amesema tarehe 17 Januri, 2022 Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya Taifa itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashuri kuu ya Taifa juu ya wagombea ambao wamejitokeza kuomba kiti hicho cha uspika.
“Tarehe 18 hadi 19 Januari kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho ambapo Kamati kuu ya Halmashauri Kuu itafanya kazi hiyo kwa eneo ambalo litaelekezwa.
“Kuanzia tarehe 21 hadi 30 Januari katika siku hizo, cocus ya chama ya wabunge wa CCM itapiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda bungeni kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania,” amesema.
Amesema itategemea kama mgombea atakuwa wa CCM au vyama vingine lakini kwa upande wa CCM mchakato wake utakamilishwa na cocus ya CCM ambayo itampata mgombea mmoja atakayepelekwa bungeni.
“Nichukue fursa hii kuwataka watanzania wote ambao wanakidhi vigezo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na CCM, kwamba wana nafasi na wana fursa kujaza nafasi hii,” amesema.
Social Plugin