Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWILI WA MWANASHERIA MKUU WA KWANZA KENYA WACHOMWA MOTO SAA 3 BAADA YA KUFARIKI...HAKUWAHI KULA UGALI UTOTONI


Mwanasheria mkuu wa kwanza wa Kenya bwana Charles Njonjo amefariki dunia akiwa na miaka 101.

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza leo Jumapili, Januari 2,2022 taarifa ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe Charles Mugane Njonjo.


"Ni kwa masikitiko makubwa kwamba asubuhi ya leo, Jumapili tarehe 2 Januari 2022, nimepokea taarifa za kuhuzunisha na za kufariki kwa Charles Mugane Njonjo," Rais Kenyatta amenukuliwa na magazeti ya Kenya.


"Kufariki kwa Mhe. Njonjo ni pigo kubwa sio tu kwa familia yake bali kwa Wakenya wote na kwa hakika, bara zima la Afrika kwa sababu ya jukumu lake kuu katika kuanzishwa kwa taifa la Kenya wakati wa uhuru," Rais alisema.

Taarifa kutoka kwa familia zinasema, maiti ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo tayari imechomwa katika mji wa Kariokor jijini Nairobi.

Familia na marafiki wa marehemu Charles Njonjo walikusanyika kwenye Tanuru ya Kihindi eneo la Kariakor jijini Nairobi.

Mwanasheria huyo mkuu wa zamani aliyehudumu baada ya Kenya kujinyakulia uhuru wake, aliaga kwa amani nyumbani kwake Muthaiga, saa kumi na moja asubuhi Jumapili Januari 2,2022.

 Kulingana na mkaza mwanawe Carey Ngini, mwili wa mwendazake ulianza kuchomwa saa nne kamili siku hiyo hiyo, kulingana na mapenzi yake na kuongeza kusema kwamba alikuwa mtu aliyeweka masharti yake wazi.

"Alikuwa wazi kuhusu kile alichotaka maishani na kile alichotaka hata baada ya kufariki dunia. Sehemu ya masharti hayo ni kuchomwa mara tu atakapoaga dunia. Hakutaka mbwembwe wala sherehe nyingi zinzoandaliwa wakati mtu mwenye staha kama yake hufanyiwa. Kama familia yake tumeheshimu uamuzi na masharti yake," aliwaambia wanahabari.

Njonjo, alikuwa mjumbe pekee aliyebaki katika Baraza la Mawaziri la uhuru wa Kenya.





Charles Njonjo ni nani?

Charles Njonjo alizaliwa na kukulia katika familia ya viongozi huku akiwa mtoto wa chifu wa ukoloni Josiah Njonjo maisha ambayo yalikuwa ndoto kwa watoto wengine wa Kiambu kuishi wakati wa ukoloni. 

Alizaliwa Januari 23, 1920 na kujiunga na shule za kifahari kanda ya Afrika Mashariki pamoja na kaka yake James.

Mwaka 1939, alijiunga na King's College Budo, na kisha baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance.

 Inaripotiwa kwamba alikula ugali mara yake ya kwanza maishani alipojiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance akidhihirisha namna aliishi maisha ya kifahari.

Baada ya elimu yake ya sekondari, alijiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare nchini Afrika Kusini na kusomea Shahada ya Kingereza na Sheria ya Afrika Kusini.

Akiwa mwingi wa maono, Njonjo alikuwa na hamu ya kusomea sheria ya Kenya lakini Waafrika hawakuwa wanaruhusiwa kusomea sheria wakati wa ukoloni.

Baada ya kufuzu katika masomo yake Afrika Kusini, Njonjo alikabidhiwa udhamini na serikali ya kikoloni kusomea Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Kusini Magharibi mwa Uingereza huko Exeter. 
Ni wakati alipokuwa nchini Uingereza, ndipo alikumbatia utamaduni wa Waingereza na kubandikwa jina "Duke of Kabeteshire" kutokana na upendo wake kwa maisha ya Ulaya.

Akiwa Uingereza, pia alisomea sheria na kurejea Kenya mwaka 1954. 

Aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mwaka 1963 wakati Kenya ilipata uhuru chini ya utawala wa hayati Jomo Kenyatta.

Taaluma yake kisiasa baada ya kutimia umri wa miaka 60, alistaafu kama Mwanasheria Mkuu na kujitosa kwenye nyanja ya kisiasa.

Alichaguliwa, bila kupingwa kama Mbunge wa Kikuyu mwaka 1980, baada ya mbunge aliyekuwepo Amos Ng'ang'a kujiuzulu.

Kulingana na mwandishi Charles Hornsby, wa kitabu Kenya: A History Since Independence, Ng’ang’a alilipwa KSh 160,000 pesa taslimu kama fidia ya kujiuzulu kwake ili kumpa Njonjo nafasi.

Baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge, Rais wa pili marehemu Daniel Moi alimteua Njonjo kushikilia wadhifa wa Waziri wa Masuala ya Kikatiba.

 Hata hivyo, alipoteza cheo mwaka 1982, kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali ili amnyanganye Moi mamlaka.

 Japo aliishi maisha ya kimya, wakati mmoja alidokeza kurejea kwenye siasa baada ya kutangaza hadharani kuunga mkono azma ya Raila Odinga kuwania urais.

Aoa akiwa na miaka 52

 Njonjo alioa mwanamke Muingereza, Margaret Bryson mwaka 1972. Hadithi hiyo iliyosimuliwa na Duncan Ndegwa, mkuu wa kwanza wa utumishi wa umma nchini Kenya, katika wasifu kuhusu jinsi Jomo Kenyatta alivyoingiwa na wasiwasi kwamba mshauri wake bado alikuwa na umri wa miaka 50.

Hii ni licha ya kuwepo na wanawake Wakenya ambao walikuwa wanmumeea mate Duke of Kabeteshire, ikidaiwa kwamba Mkuu wa Manesi Kenya, Margaret Wanjiku Koinange alikuwa amezama katika penzi la Njonjo.

Lakini Njonjo hakuzinguliwa naye kimapenzi kwani hakuwa na mpango wa kumuoa mwanamke Mwafrika na kuvunja uhusiano wake na Koinange.

 Hivyo alimuoa Margaret mwaka 1972 na kujaliwa watoto watatu pamoja na wajukuu. Njonjo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 101, wiki chache kabla ya bathdei yake ya 102.


Charles Mugane Njonjo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzaliwa wa Kenya kati ya 1963 na 1979.

Alistaafu kama mwanasheria mkuu akiwa na umri wa miaka 60.

Baadaye Njonjo alichaguliwa bila kupingwa katika Bunge la Kitaifa Aprili 1980 kama Mbunge wa Jimbo la Kikuyu.


Aliyekuwa rais Hayati Daniel Moi alimteua katika Baraza la Mawaziri mnamo Juni 1980 kuhudumu kama Waziri wa masuala ya ndani na Kikatiba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com