Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GGML KUANZA KUTUMIA RASMI UMEME WA TANESCO MWISHONI MWA 2022

Shughuli za uchimbaji zikiendelea ndani ya Mgodini wa GGML
***


 

NA MWANDISHI WETU

 

MKUU wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema mpango wa kuunganisha umeme wa gridi ya taifa kuelekea katika mgodi wa Geita Gold Mine Limited (GGML) unaendelea ambapo ujenzi wa laini maalumu za kwenda mgodini zimekamilika kwa asilimia 90. 

 

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kituo kubwa cha kupoozea umeme cha Mpomvu kilichopo Mjini Geita ambapo kinauwezo wa Megawatt 90.

 

Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo jana mjini Geita kutokana na taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limeshindwa kupeleka umeme unaohitajika na mwekezaji Geita Gold Mine.

 

Akifafanua zaidi Senyamule alisema kwa upande wa Mgodi (GGML) wanaendelea na hatua za ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha msongo wa Kilovolt 33 kuwa Kilovolt 11 ndani ya mgodi wa GGML chenye uwezo wa Megawatt 40. 

 

“GGML wanatumia voltage level tofauti na inayosambazwa na TANESCO hivyo tunategemea shughuli zote mpaka December 2022 zitakamilika,” alisema.

 

Mgodi wa GGML unatumia zaidi ya MW 40 zinazozalishwa kwa kutumia jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli tangu mwaka 2018.

 

Hata hivyo, katika mipango ya TANESCO imekuwa ikitekeleza mradi huo wa Mpovu kuhakikisha inapeleke umeme wa zaidi ya MW 20 katika mgodi huo.

 

Kituo hicho cha Mpomvu chenye eneo lenye ukubwa wa takribani heka tano kitapokea umeme wa Msongo wa Kilovolt 220 na kutoa Kilovolt 33 kisha kuvinufaisha vijiji 11 vitakavyopitiwa na mradi na wakazi 1,424 walio jirani. 

 

Mikoa jirani kama Mwanza na Kagera itaweza kunufaika na umeme huu kwani ni wa kutosha.

 

Mradi huo mkubwa wa umegharimu zaidi ya Sh bilioni 50 ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na gharama nafuu.

 

Aidha, mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupooza umeme cha Geita kitawezesha Mkoa wa Geita kuwa na umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji katika sekta mbali mbali hususan  uchimbaji wa Madini na Viwanda.

 

Kwa upande wake, Kampuni ya GGML imethibitisha kuwa utaratibu wa mananuzi ya mitambo ya kupoozea umeme yaani transformers uko katika hatua ya manunuzi na ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika kufika November 2022.

 

Makamu Rais wa Kampuni hiyo, Simon Shayo amesema GGML imekamilisha majadiliano na kuandaa rasimu ya mkataba wa kuuziana umeme (power selling agreement) na TANESCO ili kuhakikisha kampuni hiyo inapata umeme wa uhakika na kwa ubora unaotarajiwa ili kuepuka kuathiri shughuli za uzalishaji kwa Kampuni.


Shughuli za uchimbaji zikiendelea ndani ya Mgodini wa GGML

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com