Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MREMBO AREKODI TANGAZO JUU YA GHOROFA REFU KULIKO YOTE DUNIANI...MAZINGIRA HATARI YA KUTISHA



Picha na video zinazomuonesha mwanamke akirekodi tangazo la Shirika la Ndege la Fly Emirates la Dubai, zimezusha gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, kutokana na jinsi mwanamke huyo alivyoonesha ujasiri mkubwa wa kurekodi tangazo katika mazingira hatari na ya kutisha.

Mwanamke huyo, Nicole Smith-Ludvik anaonekana katika video hiyo akiwa amevalia sare za wafanyakazi wa shirika hilo huku mkononi akiwa ameshika bango linalosomeka ‘We Fly Better’ akiwa juu kabisa ya ghorofa refu kuliko yote duniani, Burji Khalifa na muda mfupi baadaye, ndege kubwa ya Airbus A380, inaonekana ikipita nyuma yake.

Mwisho wa tangazo, mwanamke huyo anaonekana akiwapungia mikono marubani wa ndege hiyo ambao nao wanaonekana vizuri wakiwa ndani ya ndege, wakiuzunguka mnara huo wenye urefu wa mita 828 kutoka usawa wa bahari.

Hii si mara ya kwanza kwa Nicole kufanya tangazo kama hilo, mwaka 2021, alionekana kwenye tangazo lingine la Emirates akiwa juu ya mnara huo lakini tofauti na safari hii, hakukuwa na ndege kwenye tangazo hilo la awali.

Wachangiaji wengi katika mitandao ya kijamii, wameshangazwa na ujasiri wa mwanamke huyo kwani ni watu wachache sana ambao mpaka sasa wameshafika juu kabisa ya mnara huo mrefu na tofauti na wengine wanaofika katika eneo hilo ambao huonekana wakiwa na hofu kubwa, uso wa Nicole unaonesha kujawa na tabasamu muda wote.

Inaelezwa kwamba, katika maisha yake ya kawaida, Nicole ambaye ni raia wa Uingereza, ni mtaalamu wa skydiving, michezo ya kuruka kutoka umbali mrefu angani lakini pia ni mwalimu wa Yoga, mambo yanayotajwa kumsaidia kutekeleza jukumu hilo kwa urahisi huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.

Katika akaunti yake ya Instagram yenye wafuasi wapatao 17,000, Nicole amekuwa akiposti picha na video mbalimbali zinazomuonesha akishiriki kwenye mchezo wa skydiving pamoja na video akiwa anafanya mazoezi ya Yoga!

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com