Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog, DODOMA.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameridhishwa na ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Intracom Fertilizer Limited ambacho kitaajiri wafanyakazi 3,000 kitakapokamikika .
Kiwanda hicho kinajengwa na mwekezaji kutoka nchini Burundi kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 180.
Hayo yamejiri leo katika ziara yake ya kutembelea ujenzi wa Kiwanda hicho kinachojengwa eneo la uwekezaji Nala Jijini Dodoma kinachotarajiwa kukamilika
baada ya miezi sita na kuanza kuzalisha mbolea.
" Tunataka tulishe Afrika Mashatiki, Nchi za Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika, (SADC ) Afrika nzima kuchukua chakula Tanzania tunaweza kuwa na hazina kubwa ya mahindi na mpunga" amesema.
Amesema lazima kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika wa mbolea ili wakulima wawe na uhakika wa uzalishaji.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya ziara Burundi kwa lengo la kuboresha uwekezaji,zaidi ya dola milioni.450 zinatumika kwa ajili kuagiza mbolea nje ya Nchi,mkakati wa Rais ni kulinda fedha zibaki Nchini," amesema
"Huu ni uwekezaji mkubwa sana nchini kwetu,Kampuni hii ina kiwanda kingine Burundi,niliwahi kufika kwenye Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha Tani 150,000 lakini kwa hapa Tanzania kitazalisha tani 600,000, mahitaji ya mbolea ni makubwa tunataka kuimarisha sekta ya kilimo .," amesema.
Amesema serikali itahakikisha mbolea yote inapatikana ndani ya nchi ili kuokoa fedha kiasi cha dola milioni 450 ambazo hutumika kwa ajili ya kuzalisha mbolea.
Pia ametaka kuwepo na mipango endelevu ya kujenga Barabara ya lami itakayofika eneo la Kiwanda hicho ili iweze kufikika kwa urahisi.
Licha ya hayo ametumia nafasi hiyo kuelekeza wizara husika kufanya utaratibu wa kuboresha miundombinu ya maji Kiwandani hapo na kueleza kuwa hali hiyo itaongeza tija ya uzalishaji wa mbolea.
"Watanzania wanaofanya kazi ya ujenzi Kiwandani hapa mnapaswa kuwa na utayari wa kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza changamoto ya ajira Tanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mahitaji ya mbolea ni tani.700,000 na kiasi cha dola milioni 450 hutumika kuagiza mbolea nje ya nchi
Amesema mbolea itakayozalishwa Kiwandani hapo itakuwa na chokaa ili hutumika kutibu udongo ambao una asidi nyingi hali itakayopelekea kuongeza mazao.
Amesema sasa bei ya mbolea imepanda katika Soko la dunia ,mbolea aina ya DAP imekuwa ikiuzwa dola 700 hadi 800 kutoka dola.400 huku mbolea ya Urea ikiwa imepanda mara mbili .
Waziri Bashe amefafanua kuwa bei hizo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi lakini Serikali ina mikakati ya kumaliza changamoto hiyo na kueleza mikakati inaendelea ya kuwekeza Kiwanda cha Urea mkoani Lindi.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani,Hamad Masauni amewahakilishia wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza Tanzania kuwa Tanzania ni salama na itaendelea kuwa salama.
Amesema Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Idara ya Uhamiaji hawatakuwa kikwazo kuhusu suala la vibali vya ukaazi.