YAKO mambo ya kushangaza, kuchekesha na hata kuhuzunisha. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Ofisa wa Jeshi la Polisi nchini, Mrakibu (SP) Patrick Kimaro (59), maarufu kama Sabasita, kuchimba kaburi lake atakalozikwa pindi atakapofariki dunia na kisha kulijengea.
Ujasiri kama huo ambao huchukuliwa na baadhi ya makabila kama uchuro, kwa ‘Sabasita’ limekuwa la kustaajabisha kwa kuwa ameanza kufanya maandalizi ya mazishi yake na kulifunika kaburi, huku akitoa ujumbe mzito kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa ujumla.
Sabasita alisema amechukua uamuzi huo mgumu akiwa na akili timamu na afya njema bila ya kushawishiwa na mtu yeyote baada ya kutafakari na kujiridhisha kwamba hatakuwa amefanya kosa lolote kwa mujibu wa sheria za nchi.
Sabasita, ambaye kwa sasa anafanya kazi Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, kwa asili ni mwenyeji wa kijiji cha Mbosho, Kata ya Masama Kati, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
“Nimefikia hatua hiyo baada ya kubaini kwamba ninaweza kukumbana na kifo wakati wowote kulingana na changamoto ninazopitia. Lakini kulingana na maandiko matakatifu ambayo yanaelekeza kila mmoja kufanya maandalizi ya kifo chake.
“Sijavunja sheria za imani ya dini yangu. Nitakuwa nimetekeleza yanayonipasa. Niko vizuri kiafya na kiakili sina tatizo lolote la kipekee na kama yapo ni haya haya ya kawaida ya binadamu wote.
“Uamuzi wangu huu unaweza kuleta mshangao kwa kuwa ni jambo ambalo halijazoeleka, lakini ni la kawaida. Tunapigiwa kelele kila siku kuwa tujiandae kwani hatujui siku wala saa, hivyo mimi nimeona nianze maandalizi,” alisema.
Pia alisema huo ni mwanzo wa maandalizi ya kumaliza maisha yake ya duniani na kuanza maisha mapya ya milele na kwamba hivi sasa anamaliza marekebisho ya kaburi lake ambalo hadi sasa limegharimu Sh. milioni nne.
Baada ya kumaliza marekebisho hayo, alisema ataanza kuandaa wosia na kuweka mipango yote muhimu itakayotekelezwa na familia yake baada ya yeye kuondoka duniani.
“Nina mke na watoto wawili na kwa wazazi wangu ambao wameshatangulia, tumezaliwa sita nikiwa mtoto wa kwanza. Niko na ndugu zangu watano, nikimaliza hapa nitaandaa wosio ili kusitokee mkanganyiko baadaye. Haya ni mambo ya kawaida na tunasisitizwa kuyafanya japo wengi wetu hatufanyi,” alisema.
Sabasita alisema ikitokea akafikwa na mauti katika mazingira ambayo mwili wake hautaonekana, utachukuliwa udongo katika eneo la mwisho atakapokuwa kabla ya kifo chake na utazikwa kwenye kaburi aliloandaa.
“Baada ya kuwaeleza ndugu zangu na familia yangu, mwanzoni hawakunielewa na walihisi kwamba nimechanganyikiwa. Lakini kwa sasa, baadhi yao wameanza kunielewa hasa wale wanaomwamini Mungu.
“Hata baada ya kuwakumbusha na kuwapitisha kwenye maandiko, mke wangu na watoto pia wanaendelea kunielewa na wataendelea kunielewa. Japo mwanzoni ilikuwa mshikemshike, marafiki zangu wako wanaonielewa na wengine bado watanielewa,” alisema.
Sabasita alisema hata wafanyakazi wenzake aliowaambia kuhusu mpango wake huo, wengi wao wanafikiri ni utani lakini kwa kifupi anawaomba ndugu, jamaa, marafiki, wafanyakazi wenzake, mabosi wake na Watanzania wamwelewe kwa vile kufa ni lazima na kila mtu anapaswa kufanya maandalizi kama wanavyofanya kwa mambo mengine.
Mmoja wa ndugu wa familia yake, Grace Kimaro, alisema mwanzoni hawakuamini, lakini baada ya kuona ujenzi wa kaburi umeanza, sasa wameamini.
“Mimi mwanzoni alivyoniambia niliogopa, nikahisi kaka yangu kachanganyikiwa, lakini baada ya kuja hapa nyumbani (Mbosho) na kupata muda wa kukaa naye, nimejiridhisha kwamba hajachanganyikiwa, wala hana tatizo lolote, bali ni maamuzi yake tu na sio jambo la ajabu,” alisema Grace.
Diwani wa Masama Kati, Kandata Kimaro, ambaye ni mwanafamilia, akizungumzia uamuzi huo, alisema haoni kama ni kitu cha ajabu, tatizo ni kwamba jambo hilo halijazoeleka.
Nao viongozi wa kiroho wa kata hiyo, akiwamo Mwinjilisti Oscar Kimaro wa Usharika wa Mafeto, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alisema kitendo hicho kinaonyesha kwamba Sabasita amejitambua na ameonyesha kukubali kifo.
Mwinjilisti huyo alisisitiza kwamba uamuzi pekee wa kukifanyia maandalizi kifo chake ni suala ambalo watu wengi kwao huwa gumu.
SABASITA NI NANI?
Mwaka 1988, Sabasita alianza kazi kama askari polisi wa cheo cha kawaida cha Constebo, akipangiwa kazi katika Mkoa wa Arusha, alipodumu hadi mwaka 1995 aliporudi Chuo cha Polisi Moshi (sasa Shule ya Polisi Moshi-MPA).
Alifanya kazi Shule ya Polisi Moshi ya kufundisha hadi Novemba, mwaka huo huo, alipopewa kazi ya kuwa kiongozi wa Kikosi Maalumu cha Kudhibiti Unyang’anyi wa kutumia silaha mkoani Morogoro. Kazi aliyoifanya kwa mafanikio hadi mwaka 2012.
Mwaka 2012 hadi 2014, alipelekwa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, akiwa Kiongozi Kikosi cha Kuzuia Unyang’anyi wa Kutumia Silaha. Baadaye mwaka huo huo, alihamishiwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
Mwaka 2016 hadi 2021, alihamishiwa Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara, kama Mkuu wa Kituo cha Polisi-Kiteto. Novemba, mwaka jana, alihamishiwa Wilaya ya Babati katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, kazi anayoifanya hadi sasa. Sabasita alisema anatarajia kustaafu utumishi Februari, 2023.
Social Plugin