WANAFUNZI 907,803 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza mwaka 2022 kati yao wavulana 439,836 na wasichana 467,967.
Hayo yamesemwa leo Januari 6 ,2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa ya maandalizi na mapokezi ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza mwaka huu.
Waziri Ummy amesema idadi hiyo imepanda ikilinganishwa na wanafunzi 833,872 waliojiunga kiadato cha kwanza mwaka 2021.
“Uchambuzi unaonesha kuwa mikoa mitano yenye matarajio ya kupokea Wanafunzi wengi zaidi kwa Kidato cha Kwanza ni Dar es Salaam (78,738), Mwanza (68,725), Kagera (50,735), Mara (48,855) na Morogoro (48,515),” amesema Waziri Ummy.
Amesema kuwa orodha ya shule watakazojiunga wanafunzi hao imetolewa na kinachosubiriwa ni muda wa kujiunga na shule.
Aidha amewataka wazazi wote ambao watoto wao wamefaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu lakini hawatokwenda kwenye shule za Serikali hasa shule maalum, watoe taarifa kwa kujaza fomu maalumu kuwawezesha wale waliokosa nafasi kwenye shule hizo kupata kukiwa na nafasi.
Aidha, Waziri Ummy amesema wazazi ambao watashindwa kupeleka watoto Shuleni watachukuliwa hatua kali ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
“Ninaitaka Mikoa, isisite kuwachukulia hatua wazazi au walezi wowote ambao wanawaficha watoto wenye umri wa kwenda Shule. Na Lazima wawachukulie hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Na tunaitaka Mikoa ituletee taarifa ya hali ya uandikishaji kila Ijumaa ya mwisho wa wiki kuanzia sasa… Kesho baada ya saa 10 Jioni, naielekeza mikoa kuniletea taarifa ya hali ya Uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza.
“Maafisa Elimu wa Wilaya na maafisa Elimu wa Mikoa, watawajibika kwa suala lolote ambalo tutalibaini kwamba Shule zilizo katika Wilaya zao zinatoza ada na michango kwa ajili ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la awali na darasa la Kwanza.
“Nitoe wito pia kwa wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito wanarejea shuleni kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya Elimu ikiwa ni pamoja na waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2021,” amesema Ummy Mwalimu.
Social Plugin