Mhitimu wa kidato cha nne mwaka 2021 Shule ya Sekondari Serengeti mkoani Mara Lucas Thomas (17) amekutwa amejinyonga kwa kamba kwenye mti mrefu katika kijiji cha Buhemba Wilaya ya Butiama baada ya kuaga anaenda shambani kuvuna mahindi na matunda.
Tukio hilo ambalo limeacha gumzo na maswali yasiyo na majibu linadaiwa kutokea Januari 14 mwaka huu 2022 ikiwa ni siku moja kabla ya Necta kutangaza matokeo ya kidato cha nne ambapo alipata daraja la pili pointi 21.
Tukio hilo limethibitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo Moses Kaegele.
“Ni kweli kajinyonga bahati mbaya hakuna taarifa zozote zimetolewa kuhusu chanzo cha kujinyonga,uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu maana kama ni matokeo kafaulu vizuri,hakuna anayeshikiliwa kwa tukio hilo,”amesema.
Alex Oscar shemeji wa marehemu akiongea na Serengeti Media Centre kwa njia ya simu amesema”asubuhi hiyo akiwa na mfuko ndani kulikuwa na kamba na kudai anaenda shambani kuchuma matunda na mahindi ya kuchoma na hakuna aliyetilia shaka kwa kuwa hapakuwa na mgogoro,”amesema.
Amesema hakurudi kama walivyotarajia na wazazi wake waliuliza uliza watu bila mafanikio na januari 15 watu walimkuta amejinyonga kwa kamba kwenye mti mrefu ambao uliwashinda hata polisi kupanda.
“Chini ya mti walikuta viatu na miwani ambayo alipendelea kuvaa,ilibidi watu wenye utaalamu wa kukwea miti mirefu wasaidie maana askari walishindwa,kumtoa huyo ilibidi wawe wanashusa taratibu kwa kamba nyingine aliyofungwa maana ni mti mrefu sana ambao kila mtu anajiuliza aliwezaje kupanda,tulimzika Januari 15,”amesema.
Mmoja wa ndugu zake amesema,Thomas ambaye ni kijana wa mwish kuzaliwa kwake alikuwa anaishi Mugumu na ameenda kwao hivi karibuni kwa ajili ya kuwasalimia,na kila mmoja hajui sababu za maamuzi hayo kwa kuwa hakuacha ujumbe wowote.
Gozbert Kusekwa ni mmoja wa walimu waliowahi kumfundisha Serengeti Sekondari amekiri kupata taarifa za kifo chake,kuhusu tabia yake amesema,”hakuwa na makuu na alikuwa mtu makini na mkimya sana,”amesema
Chanzo- Serengeti media centre