VIDEO ya mwanamke mmoja akidansi imesambaa kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha mwanamke huyo mwenye watoto watatu kupewa talaka na mumewe huku pia waajiri wake wakimfukuza kazi.
Video hiyo ya Aya Youssef mwenye umri wa miaka 30 na mwalimu wa shule ya msingi inamwonyesha akiwa amevaa kitambaa kichwani, blausi yenye mikono mirefu na kaptura ndefu huku akila densi na walimu wenzake na kufurahia safari yao ndani ya Mto Nile.
Talaka hiyo na kufutwa kazi kwa mwalimu huyo ambaye ni raia wa Misri na kumezua mjadala mkali kuhusu haki za wanawake nchini humo. Wakosoaji wanatuhumu kukiuka itikadi za dini ya Uislamu huku wengine wakisimama naye kumtetea.
Katika mahojiano na runinga moja ya kibinafasi, Bi. Youssef alisema kuwa alikuwa mwingi wa furaha akiwa katika ziara hiyo na kwamba miondoko yake ya densi alijikuta tu akijiachia bila hata yeye kujua. Walimu wengine pia walikuwa wakisakata densi pembeni mwa boti hiyo na hata kurusha mikono yao hewani. “Sote tulikuwa tunasakata densi,” alisema Bi. Youssef.
Baada ya video hiyo kusambaa mitandaoni, baadhi ya walioitazama walikuwa na misimamo mikali wakimtaja mwanamke huyo kama aliyepotoka kimaadili.
Jihad al-Qalyubi aliyetumia mtandao wa Twitter alitaja kitendo cha mwalimu huyo kuwa cha aibu huku Ahmed al-Beheiry akisema kuwa hawezi kuvumilia kumwona mwanamke aliyeolewa akisakata densi kwa namna ile.
Kwa miaka kadhaa sasa, taifa la Misri limeshuhudia visa vingi vya wanawake kushambuliwa kwenye mitandao ya kijamii huku wito wa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria ukitolewa na wanaokwazwa na hulka hiyo.
Social Plugin