Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, DODOMA.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaapisha Mawaziri,Manaibu Mawaziri,Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu Ikulu Chamwino Jijini Dodoma huku akiwapa kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi na aliyekuwa Waziri wa Katika na sheria Prof. Palamagamba Kabudi.
Akizungumza leo Jumatatu Januari 10, 2022 mara baada ya kuwaapisha Viongozi hao,Rais Samia amesema Lukuvi hatogombea nafasi ya uspika na badala yake atampa kazi maalum huku akiwaelezea Viongozi hao wawili kama Kaka zake kutokana na uzoefu wao katika kazi na kwamba hawezi kuwaacha pembeni.
Pia,ametangaza kumpa kazi aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba,Profesa,Paramagamba Kabudi ya kusimamia mikataba ambayo Serikali itaingia na wabia
Hivi karibuni Rais Samia alifanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kutowateua Lukuvi na Prof Kabudi hatua ambayo ilizua minongono kwa baadhi ya watu.
“Nina Kaka zangu wawili Lukuvi (William) na Kabudi (Paramagamba) nikiwatizama hawa age yao kama yangu na ukitizama niliowateua hamfanani kabisa kwa hiyo kaka zangu wawili hawa nimewavuta waje kwangu waje wanisaidie.
Amesema Kabudi amefanya kazi nzuri kusimamia mazungumzo ya Serikali katika mikataba hivyo amemkabidhi rasmi kazi hiyo licha ya kwamba haipo katika mfumo na kuongezà kuwa mashirika yote kazi zake ambazo zitaingia ubia na Serikali Kabudi ataongoza yote na yeye ndio Baba wa mikataba
“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ambayo sasa nataka kumkabidhi kindaki ndaki aendelee na kazi hiyo ila kazi yake kwa sababu haipo katika muundo haitangazwi wala nini na yeye ndio atasimamia kazi hiyo.
Kuhusu Lukuvi Rais Samia alisema atakuwa na kazi nae hivi karibuni na huku akiwataka watu kupuuza maneno maneno yanayoendelea ya kwamba atagombea uspika.
“Kaka yangu Lukuvi yeye atakuwa na kazi na mimi mtaisikia baadae lakini namvuta Ikulu kazi yake ni kutusisimamia kwa sababu nikiwatizama hapo wote wanakaribia kustaafu miaka 2 wengine bado mna safari ndefu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na Makatibu wakuu kwahiyo nimeona message afadhali Lukuvi katoka hajatoka yupo.
“Wengine wameanza kumletea message za ajabu ajabu wakijua atagombea uspika,hatagombania anakazi na mimi kwahiyo hatakuwa Spika wala hatagombania kwahiyo msianze kumchafua ametumikia Taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu mwache aende na mimi amalize kazi,”amesema.
Kwa upande wake,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa amemuahidi Rais Samia yeye na walioapishwa jana kwamba watafanya kazi kwa matokeo chanja kama anavyotaka kuhakikisha wanawafikia na kuwahudumia wananchi mpaka katika maeneo ya vijijini.
Pia amemuahidi kwamba watafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo na wao waliopewa dhamana wanafanya kazi kwa weledi.
“Mheshimiwa Rais mara kadhaa umekuwa ukisisitiza kufanya kazi kwa matokeo chanya naomba nirudie kukuhakikishia kwamba kwenye mipango yetu na majukumu yetu tutahakikisha tunafanya kazi kwa matokeo chanja kuwatumikia wananchi na tunajua jukumu letu la kwenda kuwakuta wananchi mpaka kijijini kwenda kuwasikiliza wananchi kule walipo na changamoto na kuwahudumia jukumu hilo tutalitekeleza,”amesema.
Kwa upande wake,Naibu Spika wa Bunge,Dk.Tulia Ackson amesema Rais Samia sio tu kiongozi wa Serikali lakini ni Mkuu wa Nchi, kwa hiyo uongozi wake hauko sawa sawa na kiongozi yeyote wa Muhimili wowote uliopo hapa nchini.
Amesema wao kama Bunge wapo tayari kutoa ushirikiano kwake
“Natoa ushauri kwenu kuwa Mhe. Rais Samia amewaamini kumsaidia, hizo kazi ni kazi zake hivyo ninyi mnapoenda kuzifanya kazi hizo fanyeni kama wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.
“Kila mmoja ambaye ameteuliwa katika nafasi yoyote aliyoipata, Mhe. Rais Samia alishafanya kazi katika maeneo hayo kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali, ninawapongeza kwa sababu mnayo sehemu ya kuanzia katika kuelezea mazuri ya Serikali hii,”alisema.
Naye,Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mahakama Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wizara zote hasa wizara inayohusiana na teknolojia iweze kwenda kwa kasi, isiwe na vizuizi wala masharti mengi ili kuweza kukuza uchumi kwa kutumia TEHAMA.
“Nawapongeza kwa imani ambayo mmepata kutoka kwa Mhe. Rais Samia ya kuweza kuchangia katika kustawisha maendeleo ya wananchi, muendelee kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Katiba na kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na usalama.