Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Clement Kivegalo (kulia),akibadilishana Mkataba na Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Orgentum International Bi.Rose Jamese huku Waziri wa Maji Jumaa Aweso,akishuhudia utiaji saini wa Mikataba ya ununuzi wa pampu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kupitia mpango wa bajeti ya mwaka 2021-2022 iliyofanyika leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.
Waziri wa Maji nchini Juma Aweso akiongea Kwenye hafla ya utiaji Saini Mkataba wa makubaliano baina ya Ruwasa na wazabuni Wazawa.
***
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1blog, DODOMA.
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) umesaini mkataba na wazabuni Wazawa ya ununuzi wa pampu za maji 310 zinazolenga kufungwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Katika Mkataba huo,jumla ya kampuni 4 zimepewa zabuni huku moja ikiwa na kandarasi mbili ambapo jumla ya Sh8.89 bilioni zitatumika kununua mashine na kurahisisha upatikanaji wa maji.
Kutokana na hayo Waziri wa Maji Juma Aweso ameagiza wazabuni wa Maji kufanya kazi kwa muda na mkataba walivyokubaliana kwani Watanzania wanataka maji na siyo siasa kama ilivyozoeleka.
Aweso ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ununuzi wa pampu za maji 310 zinazolenga kufungwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Aweso amesema wakati uliopo si wa kuweka maneno kwenye miradi ya maji bali iwe ni vitendo zaidi ili Serikali ijivunie kufanya kazi na wakandarasi Wazawa.
"Lakini kwa upande wenu Ruwasa na sisitiza malipo kwa wakati, siyo mtu amefanya kazi halafu anaendelea kudai malipo yake wakati poshi la mama limetema, haki iende na wajibu," amesema Aweso.
Kwa upande mwingine kiongozi huyo ameagiza kuanzia sasa pampu zifungwe katika maeneo yanayotoa maji hata kabla ya kujengwa kwa matenki ili wananchi waanze kunufaika kuliko kusubiri ujenzi wa matenki ambao huchukua muda mrefu kukamilika.
Kuhusu miradi ya maji ametaka sasa watupie macho mkoa wa Tanga baada ya kuwa wamemaliza Katavi, Rukwa na Songwe ambako ameshindwa kuzindua miradi yote kutokana na wingi wake na muda alipokuwa nao.
Mkurugenzi wa Ruwasa Clement Kivegalo amesema wazabuni waliopewa kazi hiyo watafanya kwa wakati kwa kuwa malipo na stahiki zote katika tenda hiyo zimekuwa tayari kinachoangaliwa ni kazi tu.
"Kwa sasa kilio cha maji kinakwenda kuwa historia katika nchi hii , tutazingatia usimamizi wa karibu wa miradi ili iwe na ubora na uendane na thamani ya fedha,"amesema.
Licha ya hayo Mkurugenzi huo amemhakikishia Waziri kuwa Ruwasa itafanya kazi usiku na mchana na karibu na wazabuni na wakandarasi bila kuchoka hadi waone wanatimiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwanamke ndoo kichwani.
Social Plugin