JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia Watu wawili wanaodaiwa kula njama na baadaye kumuua Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Barke Pesa Rashid (30) mkazi wa Ilala Utete Jijini Dar es salaam.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Muliro Jumanne amesema Barke aliuawa Januari Mosi, 2022, akiwa guest maeneo ya Tabata, ambapo mmoja wa watuhumiwa hao amekiri kutekeleza unyama huo baada ya kuahidiwa kiasi cha shilingi milioni 1.7.
Imeelezwa kuwa, chanzo cha tukio hilo ni madai ya kwamba mwanamke huyo aligharamiwa na mwanaume na akampangishia nyumba ya kuishi, lakini baadaye akaanza kumsaliti na kuwa na wanaume wengine.
“Tukio hilo limetokea Januari, Mosi,2022 Tabata Segerea kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Maridadi ambako tarehe hiyo mtuhumiwa wa kwanza Mwanaume, Jonsiner Bounser( 34), Mkazi wa Segerea Kalabash Pub alifanya mipango ya mapenzi na mwanamke aliyemuua baada ya kula njama na mtuhumiwa mwingine wa pili aliyekamatwa mwanaume anayeitwa White (33) Mfanyabiashara ya Lori la kuzolea taka Mkazi wa Tabata Segerea.
“Mwanamke huyo alikabwa shingo mpaka kupoteza maisha akiwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni, Bounser alikodiwa na White kwa malipo ya Tsh. Milioni 1.7 ili amtongoze na baadaye aende kumuua mwanamke huyo kwa madai kuwa White alimgharamia sana na kumpangishia nyumba lakini Mwanamke huyo ana wanaume wengine.
“Bounser amekiri kupewa Tsh. Milioni 1.2 kwa nyakati tofauti kabla na baada ya kutekeleza mauaji hayo na kwamba alikuwa bado anadai Tsh. 500,000 kwa White baada ya kutekeleza mauaji hayo, uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa na watafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo,”amesema Kamanda Muliro.
Social Plugin