Polisi jijini Nairobi nchini Kenya wanachunguza kisa ambapo mwanaume aitwaye Erastus Madzomba mwenye umri wa miaka 42, aliyeripotiwa kuzirai na kufariki dunia baada ya kurusha roho na mpenzi wake.
Katika kisa hicho cha Jumatano, Disemba 29,2021 Erastus Madzomba alikuwa akimumunya urojo na mpenzi wake Elgar Namusia, katika Lojing’i (Gesti) ya Broadway iliyoko kwenye Barabara ya Thiongo mtaani Kawangware.
Katika harakati hiyo, ripoti ya polisi inaeleza kwamba Namusia alidai kuwa mpenzi wake alizirai baada ya kupakua asali na kufariki dunia.
Wawili hao wamekuwa katika mahusiano kwa wiki mbili.
Kisha Namusia, aliwafahamisha maafisa wa polisi ambao walikimbia katika eneo la tukio na kupata mwili wa Madzomba kitandani.
Polisi walisema mwili huo haukuwa na majeraha yoyote na ulipelekwa katika makafani ya City ukisubiri kufanyiwa upasuaji wa maiti kubaini chanzo cha kifo chake.
Katika kisa sawia na hicho, John Gacheru alizirai ndani ya gari lake aina ya Subaru baada ya kula uroda na mwanamke aliyetambulika kama Apofia Thuita Oyego.
Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa waliokimbia katika eneo la tukio walipata mwili wa marehemu mwenye umri wa miaka 46, nje ya gari lake.
Mpenzi wake Gacheru, aliyekuwa na umri wa miaka 25, ambaye polisi walisema walikuwa katika mahusiano na marehemu kwa miaka minne, alipatikana akiwa ameketi kando ya mwili wake.
Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika Hifadhi ya maiti ya Thika General Kago ukisubiri kufanyiwa upasuaji.
Apofia anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Thika huku uchunguzi kuhusiana na kisa hicho ukiendelea.
Kwingineko mnamo Februari, mzee wa miaka 58, pia alifariki dunia baada ya kuchovya buyu la asali katika lojing’i moja Nyandarua.
Kulingana na ripoti ya polisi, Edith Wairimu Mwangi alimpata marehemu akihema sana baada ya kuenda kusafisha chumba hicho katika nyumba ya kulala wageni ya Heshima Lodge Olkalau.
Kisha mwanamke huyo wa miaka 55, alikimbia katika Kituo cha Polisi cha Olkalau kupiga ripoti ambapo maafisa wa polisi walikimbia katika eneo la tukio wakiandamana pamoja na makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Ambulensi ilitafutwa na alikimbizwa katika Hospitali ya JM Kariuki ambapo alithibitishwa kufariki.
Via Tuko News
Social Plugin