MWANAMKE mmoja, Hellen Vuyanzi (35) amejichoma moto yeye na watoto wake wawili kwa kinachodaiwa kuwa ni kutofautiana na mumewe kutokana na wivu wa mapenzi katika Kijiji cha Sirende eneo la bunge la Lugari.
Katika tukio hilo la siku ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa 2022 katika Kaunti Ndogo ya Lugari, Kakamega nchini Kenya inadaiwa kuwa mtoto wake wa tatu alinusurika katika mkasa huo baada ya kuruka nje ya nyumba kupitia dirishani.
Hellen aliripotiwa kuwa na ugomvi na mumewe na wakashauriwa na maofisa wa polisi wakiongozwa na Kamanda wa Kaunti Ndogo ya Lugari, Bernard Ngungu.
Kwa mujibu wa taarifa, baada ya kusuluhishwa, alirudi nyumbani lakini mume hakufanya hivyo ili kuepusha msuguano zaidi.
“Hellen alikuwa amemtuhumu mumewe kwa kuchepuka baada ya kubaini kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine,” alisema Kamanda Ngungu na kuongeza kuwa, huenda mwanamke huyo alinunua petroli na kuificha ndani ya nyumba kabla ya kutokea ugomvi na mumewe.
Jirani mmoja aliyekataa jina lake kutajwa, alisema wanandoa hao wamekuwa na ugomvi usioisha baada ya mwanamke huyo kuanza kumshuku mumewe. Vuyanzi walikuwa wameoana kwa miaka 12 na wenzi hao walikuwa na watoto watatu wenye umri wa miaka 11, 4 na 2.
Stephens Okila, shemeji wa marehemu, alisema alikuwa mbali na nyumbani wakati kaka yake alipompigia simu na kumwarifu kwamba aliambiwa kuwa nyumba yake inateketea.
“Tulikimbilia huko na kuthibitisha kuwa ni kweli. Kwa bahati mbaya, mke wake na watoto wawili wenye umri wa miaka 4 na 2 walikuwa tayari wamefia ndani ya nyumba. Mtoto wao mkubwa yeye alifanikiwa kujiokoa kupitia dirishani,” alisema Okila.
Okila alisema hafahamu kuhusu mzozo wowote kati ya mume na mke. “Ningesema kama kulikuwa na tatizo kati yao kwa sababu niko karibu na familia.” Ngungu alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu kifo cha mwanamke huyo na watoto wake.
Social Plugin