MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Ilanga kata ya Mlale wilayani Ileje mkoani Songwe, Subira Kibona(16) amefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni kisha mwili wake kuchomwa moto na anayesadikika kuwa mume wake, Shukrani Kamwela (16) kabla ya kutupa mabaki ya mwili huo kwenye korongo.
Kamada wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe, ASP Janeth Magomi, akizungumzia tukio hilo jana, amesema walipokea taarifa za tukio hilo juu ya mwanamke huyo ambaye alipotea nyumbani tangu Januari 13, mwaka huu.
ASP Magomi amesema baada ya kutoonekana kwa marehemu huyo wananchi walifanya juhudi za kumtafuta ndipo walipokuta mwili wake ukiwa umetupwa katika korongo lililopo katika moja ya pori mkoani humo huku ukiwa umechomwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya mgongoni na kuchomwa moto.
Hata hivyo, ASP Magomi amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na jeshi la polisi linaendelea kuchunguza na tayari linamshikilia mtuhumiwa.
Diwani wa kata hiyo, Yotamu Ndile, amesema tukio hilo limetokea Januari 13, mwaka huu saa 12 asubuhi baada ya mume wa marehemu kumwambia mke wake waende kwa Mganga wa kienyeji kutafuta dawa ya tumbo maarufu kama kata kamba kwani marehemu alikuwa na ujauzito wa miezi saba.
Aidha, akizungumza na wananchi wa eneo la tukio Afisa Tarafa ya Bulambya, Joyce Chale amewataka wananchi wa kijiji hicho kuwa na hofu ya Mungu kwani jamii inapaswa kutoa elimu kwa vijana namna ya kutatua migogoro inayojitokeza kwenye ndoa na si kukatisha uhai mtu ambaye nitegemezi kwa taifa.
Afisa huyo amewataka wananchi hao kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa za matukio kwani jeshi hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na wananchi kwa lengo la kuwakamata waharifu na kuondoa dhana ya pindi wakitoa taarifa watakamatwa.
Aidha, amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwafanya watoto wa kike kama kitega uchumi bali wawapeleke shule ili kuepusha ndoa za utotoni.
Imeelezwa kuwa tukio hilo limekuwa la pili kutokea kijijini hapo la wanawake kuchomwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni kisu huku wananchi wakiomba serikali kuchukua hatua za makusudi kukabili hali hiyo.