Tukio hilo la kinyama lilitokea Jumatatu ya Januari 17, mwaka huu huku mwili wake ukiwa umekatakatwa vipande na kuwekwa kwenye mkoba huku tukio hilo likidaiwa kufanywa na mumewe aliyefahamika kwa jina la Joseph Ngige.
Jeshi la Polisi nchini humo wamesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi, kutokana na ujumbe uliokutwa umeandikwa na kuachwa kwenye mkoba wa marehemu ukisomeka; ‘Mume wa mtu jua ni sumu’ ingawa polisi walisema huenda aliyetekeleza mauaji alitaka kuwafumba makachero macho.
Inaarifiwa Wambui aliakatiza masomo akiwa kidato cha pili na kukutana na Ngige ambaye walioana na kuenda kuishi Ruiru. Ngige ambaye ni mshukiwa katika mauaji hayo alihudhuria mazishi hayo huku baba wa marehemu akitambua mchango wa Ngige na kusema aliwasaidia pakubwa katika kushughulikia mazishi ya binti wao.
Mkuu wa kachero Ruiru, Justus Ombati, alisema maafisa wake wamepokea mazungumzo ya simu kati ya Ngige na Wambui. Ngige alimsindikiza mpenziwe kwenda kazini kabla yake kutoweka na polisi walisema hakuripoti chochote.
“Inashangaza kuwa Ngige hakuwahi ripoti kupotea kwa mkewe kwa polisi au hata kwa wenzake kazini aliona ameshindwa kurudi nyumbani siku hiyo,” Ombati alisema.
Aidha baadhi ya wafanyakazi katika hoteli alipokuwa akifanya kazi Wambu walisema walijua alikuwa na matatizo ya ndoa kutokana na machungu ya mumewe. Ngige hata hivyo amesema yeye na mkewe walikuwa ni wapenzi wa kufa kupona na hajawahi kumshuku kuwa na uhusiano wa nje.
Ripoti ya upasuaji iliyofanyia ilibaini kuwa mwili wa Esther umeonyesha alipigwa kwa kitu kizito chenye ncha butu na kunyongwa kabla ya kukatwa vipande. Vipande vya mwili wa Wambui vilipatikana katika mkoba uliowekwa nje ya kambi ya polisi wa GSU Recce Ruiru. Upasuaji ulionyesha alikosa hewa kutokana na kunyongwa na pia alikuwa na majeraha ya kugongwa na kifaa butu.
Aidha kuna ishara kuwa alidhulumiwa kingono na uchunguzi zaidi wa maabara utafanyiwa chembechembe zilizotolewa mwilini. Upasuaji ulifanyika katika makafani ya City, Ijumaa Januari 21, huku familia yake wakiongozwa na babake na mumewe Joseph Ngige wakishuhudia.
Ngige alisema mara ya mwisho kuonana ilikuwa katika kituo cha reli pale Ruiru wakati ambapo alimuaga akielekea kazini. “Jioni, nilikuwa naenda kumchukua saa mbili jioni kila siku. Hatujawahi kukosana wala mimi kumshuku kimapenzi,” alisema mumewe.
Ngige aliongeza kuwa ilifika jioni na Wambui akakosa kurudi nyumbani ambapo si jambo la kawaida. Wambui ambaye alikuwa na miaka 18 alipatikana ameuawa Jumatatu Januari 17 huku mwili wake ukiwa na michoro fulani.
Mkuu wa polisi kaunti ndogo ya Juja Dorothy Migarusha alisema kulikuwa na ishara kuwa mauaji hayo yalitokana na mzozo wa kimapenzi. Familia ya Wambui sasa inalilia haki kufanyika wakiomba polisi kuhakikisha waliohusika wamekabiliwa kisheria.