Waziri wa Habari, Mawasiliano Na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akiagana na Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania Plc, Jaji (Mstaafu) Thomas Mihayo mara baada ya kuhitimisha ziara ofisi za makao makuu ya kampuni hiyo. Picha na: TCRA
Waziri wa Habari, Mawasiliano Na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akipokelewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Beatrice Singano.
Waziri wa Habari, Mawasiliano Na Teknolojia Ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akipata maelezo ya namna huduma kwa wateja inavyotolewa katika Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom wakati wa ziara yake kwa kampuni za simu leo Januari 24,2022.
Waziri Wa Habari, Mawasiliano Na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akiagana na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya MIC Tanzania bw. Innocent Rwehabura mara baada ya kuhitimisha mkutano na menejimenti ya kampuni hiyo. Waziri nape alifanya ziara kwa kampuni tatu za simu leo Jumatatu Januari 24,2022. Picha na: TCRA
Na Mwandishi wetu
Serikali imewahakikishia watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini kwamba; itaweka mazingira rafiki yatakayowezesha kukuza uwekezaji katika sekta ya mawasiliano, ili kukuza tija kwenye sekta ya mawasiliano nchini.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nnape Moses Nnauye (Mb) katika ziara yake kwa kampuni tatu za simu nchini za Tigo, Vodacom na Airtel aliyoifanya Jumatatu Tarehe 24 Januari 2022. Waziri alisisitiza kuwa nia ya serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa, wawekezaji wanawekewa mazingira rafiki yatakayowawezesha kukuza tija katika uwekezaji wao.
“Katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, serikali ipo tayari kuboresha mazingira yakiwemo haya mazingira ya kazi yenu. Ninyi ni wadau wetu sisi ni wadau wenu, tunaweza kuzungumza, tukaaminiana, tukatengeneza mazingira mazuri zaidi; hayo mazingira tunayotaka tuyatengeneze, yatusaidie na yawashawishi muwekeze zaidi.” Alisisitiza Waziri Nnape.
“Tunao watanzania tunaowahudumia, sisi kama serikali na ninyi kama ‘operators’; wale tunaowahudumia wanatutegemea kutoa huduma nzuri, sisi huku tuwe na mahusiano mazuri ili huduma tunayoitoa iwe bora.” Waziri alisisitiza na kuongeza alipozungumza na ujumbe wa Menejimenti na Bodi ya kampuni ya Vodacom Tanzania.
Katika ziara hiyo, Waziri Nnape alipata fursa ya kuwasikiliza watoa huduma za mawasiliano ya simu kisha kufafanua kuwa, serikali imepokea changamoto kadhaa walizoainisha katika utoaji huduma na mazingira ya uwekezaji ili kuona namna itakavyozifanyia kazi na kuhakikisha zinapatiwa suluhu
Katika ziara hiyo Waziri alisisitiza umuhimu wa kampuni za simu nchini kuhakikisha zinaboresha huduma wanazotoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha ubora wa usikivu wa simu na matumizi ya data hasa kwa watumiaji wa intaneti.
“Tunaweza kuwa na mapungufu ya hapa na pale, sasa hayo mapungufu tuyaondoe hii ni meseji ya muhimu sana.” Waziri alisisitiza na kuelekeza.
Wakati wa ziara hiyo kwa nyakati tofauti Waziri alipokea taarifa za maboresho kwenye sekta ya mawasiliano kutoka kwa kampuni zote ambapo miongoni mwa maboresho hayo ni kuondoka miundombinu chakavu na kubadilisha mipya sanjari na kuhuisha teknolojia ikiwemo inayowezesha upatikanaji wa huduma kwa wateja kwa urahisi kwa kutumia programu tumizi zilizoainishwa.
“Tumejipanga kuhakikisha tunatoa huduma zenye ubora kwa wateja wetu na tutalisimamia hilo alisisitiza Beatrice Singano Afisa Habari Mwandamizi wa kampuni ya Airtel.
Wakati wa majumuisho Waziri alisisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujenga mahusiano mazuri na watoa huduma ili kuhakikisha utoaji huduma za mawasiliano kupitia kampuni hizo unakuwa bora siku hadi siku na kuongeza kuwa Wizara yake itaona namna ya kuweka mazingira bora zaidi ya ukuzaji sekta ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupitia miongozo muhimu inayoilinda sekta pana ya mawasiliano nchini.
Social Plugin