Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameeleza kushangazwa na kauli za Spika wa Bunge Job Ndugai kusimama hadharani na kukosoa mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 kutoka shirika la Fedha Duniani (IMF) wenye lengo la kuchochea mapambano dhidi ya UVIKO -19 wakati taarifa mbalimbali zinapitia kwenye bunge lake.
Akizungumza leo Jumanne Januari 4,2022 Jijini Dar es salaama wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa fedha hizo kwenye miradi mbalimbali ikiwemo elimu, afya,maji na miundombinu, Rais Samia ameonyesha kukerwa na kile alichokisema Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu Serikali kukopakopa badala ya kujiendesha kwa pesa za ndani.
“Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili, aende akasimame aseme yale. Ni stress ya 2025. Inashangaza kuona mtu mwenye uelewa, anasema kuna fedha ya tozo lakini kaenda kukopa, ya nini? Au kwa nini tunaendelea kutoa tozo wakati fedha ya mkopo ipo. Mawaziri tupeni hizo takwimu sasa hivi.
“Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kutumia kila fursa nitakayoiona itakayoletwa ambayo naweza kuitumia kuleta maendeleo Tanzania nitaitumia. Sifanyi kwa ajili ya uchaguzi wa 2025, nafanya nimeapa kuleta maendeleo kwa Watanzania.
“Nawashukuru wenyeviti wa CCM kwa kusimama na kutetea mkopo ulioleta maendeleo kwenu. Walipotokea wakuhoji mlisimama mkajibu, mkijua kwamba kinachofanyika ni utekelezaji wa ilani. Sasa mna mambo ya kwenda kifua mbele kwa wananchi kuwaambia CCM imefanya.
“Hizi Fedha zitalipwa na wananchi kupitia tozo lakini wananchi wanatakiwa kuona matunda yake. “Na kwa maana hiyo ile hamu yao na tamanio lao la 2025 ‘somehow’ tamaa zinaondoka,” amesema Rais Samia.
"Tuna serikali ya kukopa kopa tangu uhuru.
Tumekopa kopa na maendeleo tuliyopata yanatokana na kukopa kopa..kukopa siyo kioja. Tutakopa mikopo isiyo na riba ili tupate maendeleo".
"Mtu na akili yake anasimama na anahoji kuhusu mikopo na tozo, sio lolote ni homa ya 2025, kwa mtu ambaye nilimtegemea kushirikiana naye kwenye maendeleo, sikutegemea kama angesimama na kusema maneno hayo. Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili, aende akasimame aseme yale. Ni stress ya 2025", amesema Rais Samia.
"Kinachotokea sasa ni 2025 Fever, wasameheni...Haya ninayofanya sasa sifanyi kwa ajili ya mwaka 2025, nafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi...Tunachotazama sasa ni maendeleo kwa watanzania... Kelele za wanaopiga kelele hazinisumbui..mimi sivunjiki moyo, mimi nina moyo wangu, moyo wangu siyo wa glasi,ni wa nyama ulioumbwa na Mungu, hivyo sivunjiki moyo...Nishikeni mkono twende sote.
"Nataka niwaambie nitatoa list mpya ya Mawaziri hivi karibuni, wale wanaotaka kwenda na mimi nitaenda nao ila wale wanaotumika nitawapa nafasi wakatumike huko nje wanapopataka. Wale ninaohisi wanaweza kwenda na mimi…nitakwenda nao. Lakini wale wote ninaohisi ndoto zao ni kule, na wanafanya kazi kwa ajili ya kule, nitawapa nafasi waende wakajitayarishe vizuri huko nje.
"Nilipopewa mamlaka haya kuna mtu alikuja na kunipa pole na hongera akasema mtu atakayekusumbua kwenye kazi yako na uongozi ni mtu shati la kijani mwenzako wala siyo wa upinzani ,Mpinzani atakutazama unafanya nini,ukimaliza hoja zao hawana maneno lakini shati wa kijani mwenzio anayetazama mbele 2025, 2030 huyu ndiyo atakusumbua , nataka niwaambie nicho kinachotokea kwa sababu huwezi kufikiria mtu mnayemuamini anashikilia mhimili aende akasema hayo..Kinachosumbua ni Stress za mwaka 2025",ameongeza Rais Samia.
"Wakati mmenikabidhi huu mzigo, nilianza kusikia lugha zinasema serikali ya mpito, serikali ya mpito bungeni huko kwa kina Kassim. Nikarudi kwenye Katiba kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi...sikuona. Nikasema 'anhaa, twendeni"- Rais Samia
“Wakatizama mtu aliyeshika kitabu kuapa, wakamfanyia tathmini, wakamfanyia yote waliyoyafanya wakampa ‘grade’ yake wakamuweka pale. Sasa yanayotokea hawaamini, kwamba yule mtu waliyempa ile thamani ndio anayafanya. Hawaamini. Uongozi huletwa na Mungu, aliyepangiwa ndiye atakayekaa"- Rais Samia
Social Plugin