Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC SHEKIMWERI ATAKA JAMII KUKOMESHA MAUAJI, WIZI

 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akiongea na wananchi wa kata ya Kikuyu(hawapo pichani)ambapo amewataka kukemea vikali vitendo viovu.

*****

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog- DODOMA.

MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kukubali kusimamia ulinzi na usalama wao kwa kushirikiana kuwabaini watu wenye viashiria vya vitendo viovu hali itakayopunguza mauaji yanayotokea mara kwa mara.


Aidha ameuagiza uongozi wa Kata ya Kikuyu kwa kushirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama kusimamia suala la usalama kutokana na kuibuka kwa vitendo vya wizi pamoja na mauaji katika eneo hilo.


Shekimweri ametoa maagizo hayo jana Jijini Dodoma wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kikuyu Kusini wakati walipokuwa wakitoa kero mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.


Aidha ametaka pia Viongozi wa dini kuhubiri suala la kuwajenga kiroho wananchi ili kuwa na hofu ya Mungu kwani hivi sasa kumekuwa na matukio ya ajabu ambayo yanatishia usalama wa maisha ya watu.


"Naomba Viongozi husika mkae mjadili haya masuala ya usalama kama ajenda wapi wakristo wanaenda kwenye jumuiya hebu muongelee na masuala ya upendo mnapokutana haiwezekani watu wanafikia hatua ya kutoana uhai suala hili halikubaliki,"amesema


Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya  amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha anatekeleza kero za wananchi hao hasa suala la fidia ya viwanja kutokana na  mashamba yao kuchukuliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo.


Pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuzingatia suala usafi wa mazingira ili kuhakikisha Jiji linakuwa na hadhi ya Makao Makuu.


"Hapo baadae nitakuja na Sheria nikikuta mazingira yako ni machafu tutakutoza faini wala hakutakuwa na mjadala na katika kuonyesha kuwa tupo makini na hilo tayari tumeajiri migambo wa Jiji kutekeleza hilo,"amesema.


Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ,Joseph Mafuru ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa wapo katika mchakato wa kuwapatia viwanja wananchi ambao mashamba yao yamechukuliwa kama fidia.


Alisema jumla ya wananchi  328 wa Kata ya Kinyambwa wa Jijini hapa watapatiwa viwanja kama fidia  kwa  mashamba yao yalichukuliwa na Jiji kwa ajili ya uendelezaji wa Jiji hilo.


Mafuru  alisema mpaka hivi sasa tayari wameshatoa viwanja 25 kati ya 328 ambapo zoezi la upimaji linaendelea ili kuweza kukamilisha haraka na kugawa viwanja hivyo.


Awali baadhi ya wakazi hao wameeleza kero zinazo wakabili wamesema waliahidiwa na Jiji hilo kupewa viwanja mbadala baada ya kuwachukulia mashamba yao lakini mpaka sasa  bado hawajapewa.


"Mheshimiwa Mkurugenzi tunaomba uliangalie  suala hili kwa umakini kwani imekuwa ni muda mrefu sasa hatuoni kinachoendelea kuhusiana na suala hili la kupatiwa haki zetu,"walisema.


Pia wamelalamikia kitendo cha baadhi ya watu  kutupa taka ovyo katika maeneo ya makazi ya watu bila kuchukuliwa hatua na kutaka suala hilo kutatuliwa kwani ni kero kwao inayoweza kusababisha maradhi ya magonjwa ya mlipuko.


"Huu ni msimu wa mvua ,hali ya uchafu imezidi kuwa mbaya zaidi,takataka kila kona,tunaomba Mkurugenzi utusidie suala hili la sivyo magonjwaya mlipuko yatatumaliza,"wamesema baadhi ya wananchi hao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com