MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Josephine Boniface (30), Mkazi wa Kijiji cha Lyowa Mkoani Mtwara, amejeruhiwa kwa kukatwa na mapanga kwenye miguu yake yote miwili na mumewe baada ya kupoteza simu ndogo (Kiswaswadu) yenye thamani ya Tsh. 24,000.
Akizungumzia tukio hilo, Bi. Josephine amesema wakiwa kwenye sherehe za ngoma za jando na unyago usiku kijijini hapo, mumewe alimkabidhi simu hiyo ndogo ili amhifadhie lakini baadaye alipokea taarifa ya kushtukiza ya kuunguliwa moto nyumba ya mdogo wake katika kijijini jirani na kujikuta anapoteza simu bila kujua.
“Tuliporudi nyumbani, nilimwambia mume wangu kwamba simu imepotea, alipata hasira kisha akachukua panga na kuanza kunipiga nalo sehemu mbalimbali za mwili na kunijeruhi miguuni.
“Mume wangu alipofika nyumbani hapa kwa mama, tukampa taarifa za tukio la kuunguuliwa kwa moto nyumba ya ndugu zetu na mimi ndio nikamwambia kwamba nimedondosha simu.
“Akasema ‘aah haiwezekani kudondosha simu yangu mimi nataka simu yangu, sijui habari za moto, wala habari za nini, sitaki chochote, nataka simu yangu’, akaanza kunipiga,” amesema Bi. Josephine ambaye anauguza majeraha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lyowa, Mohamed Mmunda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Mwanaume huyo ametoroka baada ya tukio.
Social Plugin